< Zaburi 78 >

1 Watu wangu, sikieni mafundisho yangu, sikilizeni maneno ya kinywa changu.
Utenzi wa Asafu. Enyi watu wangu, sikieni mafundisho yangu, sikilizeni maneno ya kinywa changu.
2 Nitafungua kinywa changu katika mifano; nitaimba kuhusu mambo yaliyofichika yahusuyo yaliyopita.
Nitafungua kinywa changu kwa mafumbo, nitazungumza mambo yaliyofichika, mambo ya kale:
3 Haya ni mambo ambayo tumeyasikia na kujifunza mambo ambayo mababu zetu wametuambia sisi. Hatutawaficha uzao wao.
yale ambayo tuliyasikia na kuyajua, yale ambayo baba zetu walituambia.
4 Tutawaambia kizazi kijacho kuhusu sifa anazostahili Yahwe kwa matendo yake, nguvu zake, na maajabu ambayo ameyafanya.
Hatutayaficha kwa watoto wao; tutakiambia kizazi kijacho matendo yastahiliyo sifa ya Bwana, uweza wake, na maajabu aliyoyafanya.
5 Kwa kuwa yeye alianzisha agano la amri katika Yakobo na sheria maalumu katika Israeli. Yeye aliamuru mababu zetu kuwa walipaswa kuzifundisha kwa watoto wao.
Aliagiza amri kwa Yakobo na akaweka sheria katika Israeli, ambazo aliwaamuru baba zetu wawafundishe watoto wao,
6 Aliamuru hivi ili kwamba kizazi kijacho kiweze kuzijua amri zake, ili wawafundishe wana ambao bado hawajazaliwa.
ili kizazi kijacho kizijue, pamoja na watoto ambao watazaliwa, nao pia wapate kuwaeleza watoto wao.
7 Kisha wangeweka tumaini lao katika Mungu na kutokusahau matendo yake bali wazishike amri zake.
Ndipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu, nao wasingesahau matendo yake, bali wangalizishika amri zake.
8 Ndipo wasingekuwa kama mababu zao, ambao walikuwa wakaidi na wenye uasi, kizazi ambacho mioyo yao haikuwa kamilifu, na ambao roho zao hazikuwa na nia thabiti na aminifu kwa Mungu.
Ili wasifanane na baba zao, waliokuwa kizazi cha ukaidi na uasi, ambao roho zao hazikuwa na uaminifu kwake, ambao roho zao hazikumwamini.
9 Waefraimu walikuwa na silaha na upinde, lakini walikimbia siku ya vita.
Watu wa Efraimu, ingawa walijifunga pinde, walikimbia siku ya vita.
10 Hawakutunza agano na Mungu, na walikataa kutii sheria yake.
Hawakulishika agano la Mungu na walikataa kuishi kwa sheria yake.
11 Walisahau matendo yake, mambo ya ajabu ambayo yeye amewaonesha wao.
Walisahau aliyokuwa ameyatenda, maajabu aliyokuwa amewaonyesha.
12 Walisahau mambo ya ajabu aliyofayafanya machoni pa mababu zao katika nchi ya Misri, katika ardhi ya Soani.
Alitenda miujiza machoni mwa baba zao, huko Soani, katika nchi ya Misri.
13 Aliigawa bahari na akawaongoza katikati ya bahari; aliyafanya maji yasimame kama kuta.
Aliigawanya bahari akawapitisha, alifanya maji yasimame imara kama ukuta.
14 Wakati wa mchana aliwaongoza kwa wingu na usiku wote kwa nuru ya moto.
Aliwaongoza kwa wingu mchana na kwa nuru kutoka kwenye moto usiku kucha.
15 Alipasua miamba jangwani, na aliwapa maji mengi, ya kutosha kujaza vina virefu vya bahari.
Alipasua miamba jangwani na akawapa maji tele kama bahari,
16 Alifanya maporomoko ya maji kutiririka tokea mwambani na aliyafanya maji yatiririke kama mito.
alitoa vijito kutoka kwenye jabali lililochongoka, akayafanya maji yatiririke kama mito.
17 Lakini bado waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi dhidi ya Aliye Juu katika jangwa.
Lakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana.
18 Walimjaribu Mungu mioyoni mwao kwa kuomba chakula cha kuwatosheleza hamu zao.
Kwa makusudi walimjaribu Mungu, wakidai vyakula walivyovitamani.
19 Waliongea dhidi ya Mungu; walisema, “Kweli Mungu anaweza kuweka meza ya chakula kwa ajili yetu jangwani?
Walinena dhidi ya Mungu, wakisema, “Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani?
20 Tazama, wakati alipoupiga mwamba, maji yalibubujika, mito ikafurika. Lakini anaweza kutoa mkate tena? Ataweza kuleta nyama kwa watu wake?”
Alipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu, vijito vikatiririka maji mengi. Lakini je, aweza kutupa chakula pia? Je, anaweza kuwapa watu wake nyama?”
21 Yahwe aliposikia haya, alikasirika; moto wake uliwaka dhidi ya Yakobo, hasira yake ikamshambulia Israeli,
Bwana alipowasikia, alikasirika sana, moto wake ukawa dhidi ya Yakobo, na ghadhabu yake ikawaka dhidi ya Israeli,
22 kwa sababu hawakumwamini Mungu na hawakuamini katika wokovu wake.
kwa kuwa hawakumwamini Mungu, wala kuutumainia ukombozi wake.
23 Lakini yeye bado aliziamuru mbingu juu na kufungua milango ya mbingu.
Hata hivyo alitoa amri kwa anga zilizo juu na kufungua milango ya mbingu,
24 Aliwanyeshea mana ili wale, na aliwapa nafaka kutoka mbinguni.
akawanyeshea mana ili watu wale; aliwapa nafaka ya mbinguni.
25 Watu walikula mikate ya malaika. Aliwatumia chakula kingi.
Watu walikula mkate wa malaika, akawatumia chakula chote ambacho wangeliweza kula.
26 Alisababisha upepo wa mashariki kupiga mawinguni, na kwa uweza wake aliuongoza upepo wa kusini.
Aliachia upepo wa mashariki kutoka kwenye mbingu na kuuongoza upepo wa kusini kwa uwezo wake.
27 Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, na ndege kama wingi wa mchanga wa baharini.
Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, ndege warukao kama mchanga wa pwani.
28 Walianguka katikati ya kambi yao, na maeneo yote karibu na hema zao.
Aliwafanya washuke ndani ya kambi yao, kuzunguka mahema yao yote.
29 Hivyo walikula na walishiba. Maana aliwapa kile walichokitamani sana.
Walikula na kusaza, kwa maana alikuwa amewapa kile walichotamani.
30 Lakini walikuwa bado hawajatosheka; chakula chao kilikuwa bado kinywani mwao.
Kabla hawajamaliza kula walichokitamani, hata kilipokuwa kingali bado vinywani mwao,
31 Ndipo hasira ya Mungu iliwashambulia na kuwaua wenye nguvu kati yao. Aliwaangusha chini vijana wa Israeli.
hasira ya Mungu ikawaka juu yao, akawaua wale waliokuwa na nguvu zaidi miongoni mwao, akiwaangusha vijana wa Israeli.
32 Licha ya hili, waliendelea kutenda dhambi na hawakuyaamini matendo yake ya ajabu.
Licha ya haya yote, waliendelea kutenda dhambi, licha ya maajabu yake, hawakuamini.
33 Hivyo Mungu alizikatisha siku zao; miaka yao ilijawa na hofu.
Kwa hiyo akamaliza siku zao katika ubatili na miaka yao katika vitisho.
34 Wakati wowote Mungu alipowataabisha, nao waligeuka na kumtafuta yeye kwa bidii.
Kila mara Mungu alipowaua baadhi yao, waliosalia walimtafuta, walimgeukia tena kwa shauku.
35 Walikumbuka kuwa Mungu alikuwa mwamba wao na kuwa Mungu Aliye Juu Sana alikuwa mwokozi wao.
Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa Mwamba wao, kwamba Mungu Aliye Juu Sana alikuwa Mkombozi wao.
36 Lakini walimsifia tu kwa vinywa vyao na kumdanganya kwa maneno yao.
Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, wakisema uongo kwa ndimi zao,
37 Maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, na hawakuwa waaminifu kwa agano lake.
mioyo yao haikuwa thabiti kwake, wala hawakuwa waaminifu katika agano lake.
38 Lakini yeye, kwa kuwa alikuwa alikuwa na huruma, aliwasamehe uovu wao na hakuwaangamiza. Ndiyo, wakati mwingi aliizuia hasira yake na hakuionesha ghadhabu yake yote.
Hata hivyo alikuwa na huruma, alisamehe maovu yao na hakuwaangamiza. Mara kwa mara alizuia hasira yake, wala hakuchochea ghadhabu yake yote.
39 Alikumbuka kuwa waliumbwa kwa mwili, upepo ambao hupita nao haurudi.
Alikumbuka kwamba wao walikuwa nyama tu, upepo upitao ambao haurudi.
40 Mara ngapi wameasi dhidi yake jangwani na kumuhuzunisha nyikani!
Mara ngapi walimwasi jangwani na kumhuzunisha nyikani!
41 Tena na tena walimjaribu Mungu na wakamtilia mashaka Mtakatifu wa Israeli.
Walimjaribu Mungu mara kwa mara, wakamkasirisha yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
42 Hawakufikiria kuhusu uweza wake, jinsi alivyo waokoa dhidi ya adui
Hawakukumbuka uwezo wake, siku aliyowakomboa kutoka kwa mtesi,
43 alipofanya ishara za kutisha katika Misri na maajabu yake katika konde la Soani.
siku aliyoonyesha ishara zake za ajabu huko Misri, maajabu yake huko Soani.
44 Aligeuza mito ya Wamisri kuwa damu ili wasipate kunywa kutoka katika vijito vyao.
Aligeuza mito yao kuwa damu, hawakuweza kunywa maji kutoka vijito vyao.
45 Alituma makundi ya inzi yaliyowavamia na vyura ambao walisambaa katika nchi yao.
Aliwapelekea makundi ya mainzi yakawala, na vyura wakawaharibu.
46 Aliwapa mazao yao panzi na kazi yao nzige.
Aliruhusu tunutu kuharibu mimea yao, mazao yao kwa nzige.
47 Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe na miti ya mikuyu kwa mvua ya mawe zaidi.
Aliharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe na mikuyu yao kwa mvua iliyochangamana na theluji.
48 Aliinyeshea mifugo yao mvua ya mawe na alirusha radi ya umeme ikapiga mifugo yao. Ukali wa hasira yake ulielekea dhidi yao.
Aliwaachia mifugo yao mvua ya mawe, akayapiga makundi ya wanyama wao kwa radi.
49 Alituma gadhabu, uchungu na taabu kama wakala aletaye maafa.
Aliwafungulia hasira yake kali, ghadhabu yake, hasira na uadui, na kundi la malaika wa kuharibu.
50 Aliifanyia njia hasira yake; hakuwakinga dhidi ya kifo bali aliwakabidhi kwa pigo.
Aliitengenezea njia hasira yake, hakuwaepusha na kifo, bali aliwaachia tauni.
51 Aliwaua wazaliwa wote wa kwanza katika Misri, wazaliwa wa kwanza wa nguvu zao katika mahema ya Hamu.
Aliwapiga wazaliwa wote wa kwanza wa Misri, matunda ya kwanza ya ujana katika mahema ya Hamu.
52 Aliwaongoza nje watu wake mwenyewe kama kondoo na aliwaelekeza kupitia jangwani kama kundi.
Lakini aliwatoa watu wake kama kundi, akawaongoza kama kondoo kupitia jangwani.
53 Aliwaongoza salama na pasipo na woga, lakini bahari iliwaelemea adui zao.
Aliwaongoza salama, wala hawakuogopa, bali bahari iliwameza adui zao.
54 Kisha aliwaleta mpaka wa nchi yake takatifu, kwenye mlima huu ambao aliutwaa kwa mkono wake wa kuume.
Hivyo akawaleta hadi kwenye mpaka wa nchi yake takatifu, hadi nchi ya vilima ambayo mkono wake wa kuume ulikuwa umeitwaa.
55 Aliwafukuza mataifa mbele yao na akawapa urithi wao. Aliwakalisha makabila ya Israeli katika mahema yao.
Aliyafukuza mataifa mbele yao, na kuwagawia nchi zao kama urithi, aliwakalisha makabila ya Israeli katika makao yao.
56 Lakini bado walimjaribu na walimkaidi Mungu Aliye Juu na hawakushika amri zake takatifu.
Lakini wao walimjaribu Mungu, na kuasi dhidi ya Yeye Aliye Juu Sana, wala hawakuzishika sheria zake.
57 Hawakuwa waaminifu na walienenda katika hila kama baba zao; walikuwa sio wa kutegemewa kama upinde mbovu.
Kama baba zao, hawakuwa thabiti wala waaminifu, wakawa wasioweza kutegemewa kama upinde wenye kasoro.
58 Kwa maana walimkasirisha kwa mahali pao pa juu na walimgadhabisha hata akawa na hasira ya wivu kwa miungu yao.
Wakamkasirisha Mungu kwa mahali pao pa juu pa kuabudia miungu, wakachochea wivu wake kwa sanamu zao.
59 Mungu aliposikia hili, alikasirika na alimkataa kabisa Israeli.
Wakati Mungu alipowasikia, alikasirika sana, akamkataa Israeli kabisa.
60 Alipaacha patakatifu pa Shilo, na hema alikoishi kati ya watu.
Akaiacha hema ya Shilo, hema aliyokuwa ameiweka katikati ya wanadamu.
61 Aliruhusu nguvu zake kutekwa na kuutoa utukufu wake mkononi mwa adui.
Akalipeleka Sanduku la nguvu zake utumwani, utukufu wake mikononi mwa adui.
62 Aliukabidhi upanga watu wake, na aliukasirikia urithi wake.
Aliachia watu wake wauawe kwa upanga, akaukasirikia sana urithi wake.
63 Moto uliwavamia vijana wao wa kiume, na vijana wao wa kike hawakuwa na nyimbo za harusi.
Moto uliwaangamiza vijana wao, na wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi,
64 Makuhani wao waliangushwa kwa upanga, na wajane wao hawakulia.
makuhani wao waliuawa kwa upanga, wala wajane wao hawakuweza kulia.
65 Kisha Bwana aliamshwa kama aliyetoka usingizini, kama shujaa apigaye kelele kwa sababu ya mvinyo.
Ndipo Bwana alipoamka kama vile kuamka usingizini, kama vile mtu aamkavyo kutoka kwenye bumbuazi la mvinyo.
66 Aliwarudisha adui zake nyuma; aliwaweka kwenye aibu ya milele.
Aliwapiga na kuwashinda adui zake, akawatia katika aibu ya milele.
67 Aliikataa hema ya Yusufu, na hakulichagua kabila la Efraimu.
Ndipo alipozikataa hema za Yosefu, hakulichagua kabila la Efraimu,
68 Alilichagua kabila la Yuda na Mlima Sayuni aliyoupenda.
lakini alilichagua kabila la Yuda, Mlima Sayuni, ambao aliupenda.
69 Alipajenga patakatifu pake kama mbinguni, na kama nchi aliyoiimarisha milele.
Alijenga patakatifu pake kama vilele, kama dunia ambayo aliimarisha milele.
70 Alimchagua Daudi, mtumishi wake, alimchukua kutoka zizi la kondoo.
Akamchagua Daudi mtumishi wake na kumtoa kwenye mazizi ya kondoo.
71 Alimtoa kutoka katika kufuata kondoo pamoja na wana wao, na kumweka kuwa mchungaji wa Yakobo, watu wake, na Israeli, urithi wake.
Kutoka kuchunga kondoo alimleta kuwa mchungaji wa watu wake Yakobo, wa Israeli urithi wake.
72 Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo wake, naye aliwaongoza kwa ujuzi wa mikono yake.
Naye Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo, kwa mikono ya ustadi aliwaongoza.

< Zaburi 78 >