< Zaburi 78 >

1 Watu wangu, sikieni mafundisho yangu, sikilizeni maneno ya kinywa changu. 2 Nitafungua kinywa changu katika mifano; nitaimba kuhusu mambo yaliyofichika yahusuyo yaliyopita. 3 Haya ni mambo ambayo tumeyasikia na kujifunza mambo ambayo mababu zetu wametuambia sisi. Hatutawaficha uzao wao. 4 Tutawaambia kizazi kijacho kuhusu sifa anazostahili Yahwe kwa matendo yake, nguvu zake, na maajabu ambayo ameyafanya. 5 Kwa kuwa yeye alianzisha agano la amri katika Yakobo na sheria maalumu katika Israeli. Yeye aliamuru mababu zetu kuwa walipaswa kuzifundisha kwa watoto wao. 6 Aliamuru hivi ili kwamba kizazi kijacho kiweze kuzijua amri zake, ili wawafundishe wana ambao bado hawajazaliwa. 7 Kisha wangeweka tumaini lao katika Mungu na kutokusahau matendo yake bali wazishike amri zake. 8 Ndipo wasingekuwa kama mababu zao, ambao walikuwa wakaidi na wenye uasi, kizazi ambacho mioyo yao haikuwa kamilifu, na ambao roho zao hazikuwa na nia thabiti na aminifu kwa Mungu. 9 Waefraimu walikuwa na silaha na upinde, lakini walikimbia siku ya vita. 10 Hawakutunza agano na Mungu, na walikataa kutii sheria yake. 11 Walisahau matendo yake, mambo ya ajabu ambayo yeye amewaonesha wao. 12 Walisahau mambo ya ajabu aliyofayafanya machoni pa mababu zao katika nchi ya Misri, katika ardhi ya Soani. 13 Aliigawa bahari na akawaongoza katikati ya bahari; aliyafanya maji yasimame kama kuta. 14 Wakati wa mchana aliwaongoza kwa wingu na usiku wote kwa nuru ya moto. 15 Alipasua miamba jangwani, na aliwapa maji mengi, ya kutosha kujaza vina virefu vya bahari. 16 Alifanya maporomoko ya maji kutiririka tokea mwambani na aliyafanya maji yatiririke kama mito. 17 Lakini bado waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi dhidi ya Aliye Juu katika jangwa. 18 Walimjaribu Mungu mioyoni mwao kwa kuomba chakula cha kuwatosheleza hamu zao. 19 Waliongea dhidi ya Mungu; walisema, “Kweli Mungu anaweza kuweka meza ya chakula kwa ajili yetu jangwani? 20 Tazama, wakati alipoupiga mwamba, maji yalibubujika, mito ikafurika. Lakini anaweza kutoa mkate tena? Ataweza kuleta nyama kwa watu wake?” 21 Yahwe aliposikia haya, alikasirika; moto wake uliwaka dhidi ya Yakobo, hasira yake ikamshambulia Israeli, 22 kwa sababu hawakumwamini Mungu na hawakuamini katika wokovu wake. 23 Lakini yeye bado aliziamuru mbingu juu na kufungua milango ya mbingu. 24 Aliwanyeshea mana ili wale, na aliwapa nafaka kutoka mbinguni. 25 Watu walikula mikate ya malaika. Aliwatumia chakula kingi. 26 Alisababisha upepo wa mashariki kupiga mawinguni, na kwa uweza wake aliuongoza upepo wa kusini. 27 Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, na ndege kama wingi wa mchanga wa baharini. 28 Walianguka katikati ya kambi yao, na maeneo yote karibu na hema zao. 29 Hivyo walikula na walishiba. Maana aliwapa kile walichokitamani sana. 30 Lakini walikuwa bado hawajatosheka; chakula chao kilikuwa bado kinywani mwao. 31 Ndipo hasira ya Mungu iliwashambulia na kuwaua wenye nguvu kati yao. Aliwaangusha chini vijana wa Israeli. 32 Licha ya hili, waliendelea kutenda dhambi na hawakuyaamini matendo yake ya ajabu. 33 Hivyo Mungu alizikatisha siku zao; miaka yao ilijawa na hofu. 34 Wakati wowote Mungu alipowataabisha, nao waligeuka na kumtafuta yeye kwa bidii. 35 Walikumbuka kuwa Mungu alikuwa mwamba wao na kuwa Mungu Aliye Juu Sana alikuwa mwokozi wao. 36 Lakini walimsifia tu kwa vinywa vyao na kumdanganya kwa maneno yao. 37 Maana mioyo yao haikuwa thabiti kwake, na hawakuwa waaminifu kwa agano lake. 38 Lakini yeye, kwa kuwa alikuwa alikuwa na huruma, aliwasamehe uovu wao na hakuwaangamiza. Ndiyo, wakati mwingi aliizuia hasira yake na hakuionesha ghadhabu yake yote. 39 Alikumbuka kuwa waliumbwa kwa mwili, upepo ambao hupita nao haurudi. 40 Mara ngapi wameasi dhidi yake jangwani na kumuhuzunisha nyikani! 41 Tena na tena walimjaribu Mungu na wakamtilia mashaka Mtakatifu wa Israeli. 42 Hawakufikiria kuhusu uweza wake, jinsi alivyo waokoa dhidi ya adui 43 alipofanya ishara za kutisha katika Misri na maajabu yake katika konde la Soani. 44 Aligeuza mito ya Wamisri kuwa damu ili wasipate kunywa kutoka katika vijito vyao. 45 Alituma makundi ya inzi yaliyowavamia na vyura ambao walisambaa katika nchi yao. 46 Aliwapa mazao yao panzi na kazi yao nzige. 47 Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe na miti ya mikuyu kwa mvua ya mawe zaidi. 48 Aliinyeshea mifugo yao mvua ya mawe na alirusha radi ya umeme ikapiga mifugo yao. Ukali wa hasira yake ulielekea dhidi yao. 49 Alituma gadhabu, uchungu na taabu kama wakala aletaye maafa. 50 Aliifanyia njia hasira yake; hakuwakinga dhidi ya kifo bali aliwakabidhi kwa pigo. 51 Aliwaua wazaliwa wote wa kwanza katika Misri, wazaliwa wa kwanza wa nguvu zao katika mahema ya Hamu. 52 Aliwaongoza nje watu wake mwenyewe kama kondoo na aliwaelekeza kupitia jangwani kama kundi. 53 Aliwaongoza salama na pasipo na woga, lakini bahari iliwaelemea adui zao. 54 Kisha aliwaleta mpaka wa nchi yake takatifu, kwenye mlima huu ambao aliutwaa kwa mkono wake wa kuume. 55 Aliwafukuza mataifa mbele yao na akawapa urithi wao. Aliwakalisha makabila ya Israeli katika mahema yao. 56 Lakini bado walimjaribu na walimkaidi Mungu Aliye Juu na hawakushika amri zake takatifu. 57 Hawakuwa waaminifu na walienenda katika hila kama baba zao; walikuwa sio wa kutegemewa kama upinde mbovu. 58 Kwa maana walimkasirisha kwa mahali pao pa juu na walimgadhabisha hata akawa na hasira ya wivu kwa miungu yao. 59 Mungu aliposikia hili, alikasirika na alimkataa kabisa Israeli. 60 Alipaacha patakatifu pa Shilo, na hema alikoishi kati ya watu. 61 Aliruhusu nguvu zake kutekwa na kuutoa utukufu wake mkononi mwa adui. 62 Aliukabidhi upanga watu wake, na aliukasirikia urithi wake. 63 Moto uliwavamia vijana wao wa kiume, na vijana wao wa kike hawakuwa na nyimbo za harusi. 64 Makuhani wao waliangushwa kwa upanga, na wajane wao hawakulia. 65 Kisha Bwana aliamshwa kama aliyetoka usingizini, kama shujaa apigaye kelele kwa sababu ya mvinyo. 66 Aliwarudisha adui zake nyuma; aliwaweka kwenye aibu ya milele. 67 Aliikataa hema ya Yusufu, na hakulichagua kabila la Efraimu. 68 Alilichagua kabila la Yuda na Mlima Sayuni aliyoupenda. 69 Alipajenga patakatifu pake kama mbinguni, na kama nchi aliyoiimarisha milele. 70 Alimchagua Daudi, mtumishi wake, alimchukua kutoka zizi la kondoo. 71 Alimtoa kutoka katika kufuata kondoo pamoja na wana wao, na kumweka kuwa mchungaji wa Yakobo, watu wake, na Israeli, urithi wake. 72 Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo wake, naye aliwaongoza kwa ujuzi wa mikono yake.

< Zaburi 78 >