< Mithali 1 >

1 Mithali za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli.
Mithali za Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:
2 Mithali hizi zinafundisha hekima na maarifa, kufundisha maneno ya busara,
Kwa kupata hekima na nidhamu; kwa kufahamu maneno ya busara;
3 ili mpate maarifa kwa ajili ya kuishi kwa kutenda wema, haki na adili.
kwa kujipatia nidhamu na busara, kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;
4 Mithali hizi zinatoa hekima kwa wale ambao hawakufunzwa, na kuwapa vijana maarifa na hadhari.
huwapa busara wajinga, maarifa na akili kwa vijana;
5 Watu wenye busara wasikie na kuongeza elimu yao na watu wenye ufahamu wapate mwongozo,
wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao, wenye kupambanua na wapate mwongozo;
6 kwa kuelewa mithali, misemo, vitendawili na maneno ya wenye busara.
kwa kufahamu mithali na mifano, misemo na vitendawili vya wenye hekima.
7 Hofu ya Yehova ni chanzo cha maarifa- wapumbavu hudharau hekima na nidhamu.
Kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.
8 Mwanangu, sikia fundisho la baba yako na wala usiziache kanuni za mama yako;
Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
9 zitakuwa kilemba cha neema katika kichwa chako na jebu zinazoning'inia kwenye shingo yako.
Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako, na mkufu wa kuipamba shingo yako.
10 Mwanangu wenye dhambi wakikushawishi katika dhambi zao, kataa kuwafuata.
Mwanangu, kama wenye dhambi wakikushawishi, usikubaliane nao.
11 Kama watasema, “haya tufuatae, tuvizie ili kufanya mauaji, tujifiche ili tuwashambulie watu wasio na hatia, pasipo sababu.
Kama wakisema, “Twende tufuatane; tukamvizie mtu na kumwaga damu, njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia;
12 Haya tuwameza wakiwa hai, kama kuzimu inavyowachukua wenye afya, na kuwa kama wale waangukao kwenye shimoni. (Sheol h7585)
tuwameze wakiwa hai kama kaburi, wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni. (Sheol h7585)
13 Tutapata vitu vyote vya thamani; tutazijaza nyumba zetu vile tunavyoiba kwa wengine.
Tutapata aina zote za vitu vya thamani na kujaza nyumba zetu kwa nyara.
14 Weka vitu vyako kwetu; tutakuwa na mfuko moja kwa pamoja.”
Njoo ushirikiane nasi, vitu vyote tutakavyopata tutagawana.”
15 Mwanangu, usitembee katika njia moja pamoja nao; usiruhusu mguu wako kugusa katika mapito yao;
Mwanangu, usiandamane nao. Usiweke mguu wako katika njia zao,
16 miguu ya hukimbilia mabaya na huharakisha kumwaga damu.
kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi, ni wepesi kumwaga damu.
17 Kwa kuwa haina maana kumtegea ndege mtego wakati ndege anaona.
Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu wakati ndege wote wanakuona!
18 Watu hawa huvizia kujiua wenyewe—wanatega mtego kwa ajili yao wenyewe.
Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe; hujivizia tu wenyewe!
19 Ndivyo zilivyo njia za kila ambaye hupata utajiri kwa udhalimu; mapato ya udhalimu huondoa uhai wa wenye utajiri.
Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila; huuondoa uhai wa wale wenye mali.
20 Hekima inalia kwa sauti mtaani, inapaza sauti katika viwanja;
Hekima huita kwa sauti kuu barabarani, hupaza sauti yake kwenye viwanja vikubwa;
21 katika mitaa inalia kwa sauti kuu, kwenye maingilio ya milango ya mji inasema “
kwenye makutano ya barabara za mji zenye makelele mengi hupaza sauti, kwenye malango ya mji hutoa hotuba yake:
22 Mpaka lini enyi wajinga mtapenda kuwa wajinga? Mpaka lini enyi wenye dhihaka mtapenda dhihaka, na hadi lini enyi wapumbavu, mtachukia maarifa?
“Enyi wajinga, mtangʼangʼania ujinga wenu hadi lini? Mpaka lini wenye mizaha watafurahia mizaha, na wapumbavu kuchukia maarifa?
23 Zingatia karipio langu; nitatoa mawazo yangu kwa ajili yenu; nitawafahamisha maneno yangu.
Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu, ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu na kuwafahamisha maneno yangu.
24 Nimeita, nanyi mkakataa kusikiliza; nimeunyosha mkono wangu, wala hakuna aliyezingatia.
Lakini kwa kuwa mlinikataa nilipowaita na hakuna yeyote aliyekubali niliponyoosha mkono wangu,
25 Lakini mumedharau mafundisho yangu yote na wala hamkuzingatia maelekezo yangu.
kwa kuwa mliyapuuza mashauri yangu yote na hamkukubali karipio langu,
26 Nitacheka katika taabu yenu, nitawadhihaki wakati wa kupatwa taabu-
mimi nami nitawacheka katika maafa yenu, nitawadhihaki wakati janga litawapata:
27 hofu ya kutisha itawapata kama tufani na maafa yatawakumba kama upepo wa kisulisuli, taabu na uchungu vitawapata.
wakati janga litawapata kama tufani, wakati maafa yatawazoa kama upepo wa kisulisuli, wakati dhiki na taabu zitawalemea.
28 Halafu wataniita, nami sitawajibu; wataniita katika hali ya kukata tamaa lakini hawataniona.
“Ndipo watakaponiita lakini sitawajibu; watanitafuta lakini hawatanipata.
29 Kwa sababu wamechukia maarifa na hawakuchagua kuwa na hofu ya Yehova,
Kwa kuwa walichukia maarifa, wala hawakuchagua kumcha Bwana,
30 hawakufuata mafundisho yangu na wakayadharau masahihisho yangu yote.
kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu, na kukataa maonyo yangu,
31 Watakula matunda ya njia zao, na watashibishwa kwa matunda ya hila zao wenyewe.
watakula matunda ya njia zao, na watashibishwa matunda ya hila zao.
32 kwa maana wajinga hufa wanaporudi nyuma, na kutojali kwa wapumbavu kutawaangamiza.
Kwa kuwa ukaidi wa wajinga utawaua, nako kuridhika kwa wajinga kutawaangamiza.
33 Bali kila anisikilizaye ataishi kwa usalama na atapumzika salama pasipo hofu ya maafa.
Lakini yeyote anisikilizaye ataishi kwa usalama, atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”

< Mithali 1 >