< Zaburi 64 >

1 Sikia sauti yangu, Mungu, usikilize malalamiko yangu; unilinde dhidi ya hofu ya adui zangu. 2 Unifiche dhidi ya mipango ya siri ya wafanyao maovu, unifiche dhidi ya watendao vurugu ya udhalimu. 3 Wao wamenoa ndimi zao kama panga; wamelenga mishale yao, maneno machungu, 4 ili kwamba waweze kupiga kutoka mahali pa siri kwenda kwa mtu asiye na hatia; wampige yeye kwa ghafla nao wasihofu lolote. 5 Wao wanahamasishana wenyewe katika kupanga uovu; wanashauriana pamoja wao binafsi ili kuweka mitego; nao husema, “Ni nani atakayetuona?” 6 Wanabuni mipango ya dhambi; “Tumemaliza,” wanasema, “ni mpango makini.” Mawazo ya ndani na mioyo ya watu ni ya kina. 7 Lakini Mungu atawapiga wao; ghafla watajeruhiwa kwa mishale yake. 8 Watafanywa kuwa mashakani, kwa kuwa ndimi zao wenyewe ziko kinyume nao; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao. 9 Watu wote wataogopa na kutangaza matendo ya Mungu. Kwa hekima watafikiria kuhusu kile yeye ametenda. 10 Wenye haki watakuwa na furaha kuhusu Yahwe nao watakimbilia kwake; wote wenye haki moyoni watajivuna katika yeye.

< Zaburi 64 >