< Zaburi 96 >

1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya; mwimbieni Bwana dunia yote. 2 Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku. 3 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote. 4 Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. 5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini Bwana aliziumba mbingu. 6 Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake. 7 Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa, mpeni Bwana utukufu na nguvu. 8 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; leteni sadaka na mje katika nyua zake. 9 Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake; dunia yote na itetemeke mbele zake. 10 Katikati ya mataifa semeni, “Bwana anatawala.” Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa; atawahukumu watu kwa uadilifu. 11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake; 12 mashamba na yashangilie, pamoja na vyote vilivyomo ndani yake. Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha; 13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja, anakuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa katika kweli yake.

< Zaburi 96 >