< Zaburi 98 >

1 Zaburi. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu umemfanyia wokovu. 2 Bwana ameufanya wokovu wake ujulikane na amedhihirisha haki yake kwa mataifa. 3 Ameukumbuka upendo wake na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli; miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu. 4 Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote, ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda; 5 mwimbieni Bwana kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za kuimba, 6 kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume: shangilieni kwa furaha mbele za Bwana, aliye Mfalme. 7 Bahari na ivume na kila kiliomo ndani yake, dunia na wote wakaao ndani yake. 8 Mito na ipige makofi, milima na iimbe pamoja kwa furaha, 9 vyote na viimbe mbele za Bwana, kwa maana yuaja kuhukumu dunia. Atahukumu dunia kwa haki na mataifa kwa haki.

< Zaburi 98 >