< Zekaria 7 >

1 Mwaka wa minne wa utawala mfalme Dario, siku ya nne ya mwezi wa Kisleu(ambao ni mwezi wa tisa), neno la Yahwe lilimjia Zekaria kusema. 2 Watu wa Betheli wamemtuma Shareza, Regemu Meleki na watu wao kuomba mbele ya uso wa Yahwe. 3 Wakaongea na makuhani waliokuwa katika nyumba ya Yahwe wa majeshi na kwa manabii; wakasema, “Je niomboleze katika mwezi wa tano kwa njia ya kufunga, kama nilivyofanya miaka mingi hii?” 4 Ndipo neno la Yahwe wa majeshi liliponijia kusema, 5 “Ongea na watu wote wa nchi na makuhani uwaambie, “Mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba katika hii miaka sabini, je kweli mlifunga kwa ajili yangu? 6 Na mlipokula na kunywa, hamkula na kunywa kwa ajili yenu wenyewe? 7 Je hayo siyo maneno aliyosema Yahwe kwa vinywa vya manabii wa zamani, mlipokuwa bado mnaishi Yerusalemu na miji ya kandokando yenye mafanikio na iliyokaa Negebu, na upande wa magharibi chini ya vilima?” 8 Neno la Yahwe likamjia Zekaria kusema, 9 “Yahwe wa majeshi asema hivi, 'Hukumuni kwa haki, uaminifu wa agano, na rehema. Kila mtu na amtendee hivi ndugu yake. 10 Juu ya mjane na yatima, mgeni, na masikini - usiwanyanyase, na asiwepo miongoni mwenu anayepanga madhara yoyote dhidi ya mwingine mioyoni mwenu. 11 Lakini waliyashupaza mabega yao na hawakujari. Waliziba masikio yao ili wasisikie. 12 Waliifanya mioyo yao kuwa migumu kama mwamba ili wasiisikie sheria au neno la Yahwe wa majeshi. Alipeleka ujumbe kwa watu nyakati za zamani kwa Roho wake, kwa vinywa vya manabii. Lakini watu hawakusikia, hivyo Yahwe wa majeshi aliwakasirikia sana. 13 Hata ikawa alipoita hawakusikia. Vilevile,” asema Yahwe wa majeshi, “wataniita, lakini sitasikiliza. 14 Kwa maana nitawatawanya kwa upepo wa kisurisuri katika mataifa yote ambayo hawajawai kuyaona, na baada yao nchi itakuwa wazi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja atakayepita au kukaa katika hiyo nchi kwa kuwa wameigeuza nchi yao yenye kupendeza kuwa isiyofaa.

< Zekaria 7 >