< Ufunuo 3 >

1 Kwa malaika wa kanisa la Sardi andika: 'Maneno ya yule anayeshikilia zile roho saba za Mungu na nyota saba. “Najua ambacho umefanya. Una sifa ya kuwa hai, lakini u-mfu.
“Kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika: “Haya ndiyo maneno ya aliye na zile Roho sabaza Mungu na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, kwamba una sifa ya kuwa hai, lakini umekufa.
2 Amka na kuimarisha yaliyosalia, lakini yako karibu kufa, kwa sababu sikuyaona matendo yako yamekamilika machoni pa Mungu wangu.
Amka! Nawe uyaimarishe yale yaliyosalia na yaliyo karibu kufa, kwa maana sikuona kwamba kazi zako zimekamilika machoni pa Mungu wangu.
3 Kwa hiyo, kumbuka, yale uliyoyapokea na kusikia. Yatii na kutubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwivi, na hutajua saa ipi nitakayokuja juu yako.
Kumbuka basi yale uliyoyapokea na kuyasikia, yatii na ukatubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwizi wala hutajua saa nitakayokuja kwako.
4 Lakini kuna majina machache ya watu katika Sardi ambao hawakuchafua nguo zao. Watatembea pamoja nami, wamevaa nguo nyeupe, kwa sababu wanastahili.
“Lakini bado una watu wachache katika Sardi ambao hawajayachafua mavazi yao. Wao wataenda pamoja nami, wakiwa wamevaa mavazi meupe, kwa maana wanastahili.
5 Yeye ashindaye atavikwa mavazi meupe, na kamwe sitalifuta jina lake kutoka katika kitabu cha uzima, na nitalitaja jina lake mbele ya Baba yangu, na mbele ya malaika.
Yeye ashindaye atavikwa vazi jeupe kama wao. Sitafuta jina lake kutoka kitabu cha uzima, bali nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu na mbele za malaika wake.
6 Ukiwa na sikio, sikiliza Roho ayaambiavyo makanisa.”
Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.
7 “Kwa malaika wa kanisa la Philadefia andika: Maneno ya aliye mtakatifu na kweli - aliye na funguo za Daudi, hufungua na hakuna afungaye, hufunga na hakuna awezaye kufungua.
“Kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, yeye aliye na ufunguo wa Daudi. Anachokifungua hakuna awezaye kukifunga, wala anachokifunga hakuna awezaye kukifungua.
8 Najua ambacho umetenda. Tazama, nimekuwekea mbele yako mlango uliofunguliwa ambao hakuna awezaye kuufunga. Najua unazo nguvu kidogo, lakini umelitii neno langu na hujalikana jina langu.
Nayajua matendo yako. Tazama, nimeweka mbele yako mlango uliofunguliwa, wala hakuna awezaye kuufunga. Ninajua kwamba una nguvu kidogo lakini umelishika neno langu wala hukulikana Jina langu.
9 Angalia! Wote walio wa sinagogi la shetani, wale wasemao wao ni Wayahudi na kumbe siyo, badala yake wanadanganya. Nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, na watajua ya kuwa nilikupenda.
Nitawafanya wale wa sinagogi la Shetani, wale ambao husema kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali ni waongo, nitawafanya waje wapige magoti miguuni pako, na wakiri ya kwamba nimekupenda.
10 Kwa kuwa umetunza amri yangu kwa uvumilivu wa uthabiti, nitakulinda pia katika saa yako ya kujaribiwa ambayo inakuja katika ulimwengu wote, kuwajaribu wale wote wanaoishi katika nchi.
Kwa kuwa umeshika amri yangu ya kuvumilia katika saburi, nitakulinda katika saa ya kujaribiwa inayokuja ulimwenguni pote, ili kuwajaribu wote wakaao duniani.
11 Naja upesi. Shikilia sana kile ulichonacho ili asiwepo mtu wa kuitwaa taji yako.
“Ninakuja upesi. Shika sana ulicho nacho, ili mtu asije akaichukua taji yako.
12 Nitamfanya yeye ashindaye kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, na hatatoka nje kamwe. Nitaliandika kwake jina la Mungu wangu, jina la mji wa Mungu wangu (Yerusalemu mpya, ushukao chini toka mbinguni kwa Mungu wangu), na jina langu jipya.
Yeye ashindaye nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo kamwe. Nitaandika juu yake Jina la Mungu wangu na jina la mji mkubwa wa Mungu wangu, Yerusalemu mpya, ambao unashuka kutoka mbinguni kwa Mungu wangu. Nami pia nitaandika juu yake Jina langu jipya.
13 Yeye aliye na sikio, na asikie ambacho Roho anasema kwa makanisa.'
Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.
14 “Kwa malaika wa kanisa la Laodikia andika: 'Maneno yake aliye Amina, wakutegemewa na shahidi mwaminifu, mtawala juu ya uumbaji wa Mungu.
“Kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye Amen, shahidi mwaminifu na wa kweli, mtawala wa uumbaji wote wa Mungu.
15 Najua ambacho umefanya, na kwamba wewe si baridi wala moto, natamani kwamba ungekuwa wa baridi au moto!
Nayajua matendo yako, ya kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungelikuwa moja au lingine.
16 Hivyo, kwa sababu wewe ni vuguvugu, si moto wala baridi, nitakutapika utoke kinywani mwangu.
Hivyo kwa kuwa u vuguvugu, si baridi wala moto, nitakutapika utoke kinywani mwangu.
17 Kwa kuwa unasema, “Mimi ni tajiri, nimekuwa na mali nyingi, na sihitaji chochote.” Lakini hujui kwamba wewe ni duni sana, wakuhuzunikiwa, maskini, kipofu na uchi.
Kwa maana unasema: ‘Mimi ni tajiri, nimejilimbikizia mali, wala sihitaji kitu chochote.’ Lakini hutambui ya kwamba wewe ni mnyonge, wa kuhurumiwa, maskini, kipofu, tena uliye uchi.
18 Sikiliza ushauri kwangu: Nunua kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto ili upate kuwa tajiri, na nguo nyeupe za kumetameta ili ujivike mwenyewe na usioneshe aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka katika macho yako upate kuona.
Nakushauri ununue kutoka kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, ili upate kuwa tajiri, na mavazi meupe ili uyavae upate kuficha aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka macho yako ili upate kuona.
19 Kila nimpendaye, namwelekeza na kuwafundisha namna iwapasavyo kuishi; kwa hiyo, kuwa mkweli na kutubu.
“Wale niwapendao, ninawakemea na kuwaadibisha. Hivyo uwe na bidii ukatubu.
20 Tazama nasimama katika mlango na kubisha. Yeyote asikiaye sauti yangu na kufungua mlango, nitakuja na kuingia nyumbani kwake, na kula chakula naye na yeye pamoja nami.
Tazama! Nasimama mlangoni nabisha. Kama mtu yeyote akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia ndani na kula pamoja naye, naye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa haki ya kukaa chini pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na kukaa chini pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi.
“Yeye ashindaye nitampa haki ya kuketi pamoja nami kwenye kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na nikaketi pamoja na Baba yangu kwenye kiti chake cha enzi.
22 Yeye aliye na sikio, na asikilize ambacho Roho ayaambia makanisa.”
Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.”

< Ufunuo 3 >