< Zaburi 97 >

1 Yahwe anatawala; nchi ishangilie; visiwa vingi na vifurahi. 2 Mawingu na giza vyamzunguka. Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake. 3 Moto huenda mbele zake nao huwateketeza adui zake pande zote. 4 Taa yake huangaza ulimwengu; nchi huona na kutetemeka. 5 Milima huyeyuka kama nta mbele za Yahwe, Bwana wa dunia yote. 6 Mbingu hutangaza haki yake, na mataifa yote huuona utukufu wake. 7 Wale wote waabuduo sanamu za kuchonga wataaibishwa, wale wanao jivuna katika sanamu zisizo na maana mpigieni yeye magoti, enyi miungu wote! 8 Sayuni ilisikia na kufurahi, na miji ya Yuda ilishangilia kwa sababu ya amri zako za haki, Yahwe. 9 Kwa kuwa wewe, Yahwe, ndiye uliye juu sana, juu ya nchi yote. Umetukuka sana juu ya miungu yote. 10 Ninyi ambao mnampenda Yahwe, chukieni uovu! Yeye hulinda uhai wa watakatifu wake, naye huwatoa mikononi mwa waovu. 11 Nuru imepandwa kwa ajili ya wenye haki na furaha kwa ajili ya wanyoofu wa moyo. 12 Furahini katika Yahwe, enyi wenye haki; na mpeni shukurani mkumbukapo utakatifu wake.

< Zaburi 97 >