< Zaburi 95 >

1 Oh njoni, tumwimbie Yahwe; na tumwimbie kwa shangwe mwamba wa wokovu wetu. 2 Tuingie uweponi mwake kwa shukrani; tumwimbie yeye kwa zaburi ya sifa. 3 Kwa maana Yahwe ni Mungu mkuu na Mfalme mkuu juu ya miungu yote. 4 Mkononi mwake zimo bonde za dunia; navyo vilele vya milima ni vyake. 5 Bahari ni yake, maana aliiumba, na mikono yake ilitengeneza nchi kavu. 6 Oh njoni, tumwabudu na tupige magoti; tupige magoti mbele za Yahwe, muumbaji wetu: 7 Kwa maana yeye ni Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho yake na kondoo wa mkono wake. Ni heri leo mngesikia sauti yake! 8 Msiifanye migumu mioyo yenu, kama vile huko Meriba, au kama ile siku ya Masa jangwani, 9 ambako baba zenu walinijaribu na kunipima, japo walikuwa wameyaona matendo yangu. 10 Kwa miaka arobaini nilikasirishwa na kizazi hicho na kusema, 'Hawa ni watu ambao mioyo yao imepotoka; hawazijui njia zangu.' 11 Hivyo katika hasira yangu niliapa kwamba wasingeingia kamwe mahali pa pumziko.”

< Zaburi 95 >