< Zaburi 92 >

1 Ni jambo jema kumshukuru Yahwe na kuliimbia sifa jina lako, Uliye Juu, 2 kutangaza uaminifu wa agano lako wakati wa asubuhi na uaminifu wako kila usiku, 3 kwa kinubi cha nyuzi kumi na kwa tuni ya kinubi. 4 Kwa kuwa wewe, Yahwe, matendo yako yamenifurahisha. Nitaimba kwa furaha kwa sababu ya matendo ya mikono yako. 5 Ni jinsi gani matendo yako ni makuu, Yahwe! mawazo yako ni ya kina. 6 Mtu mpumbavu hawezi kuyajua, wala mjinga kuyaelewa haya: 7 Wasio haki watakapochipuka kama nyasi, na hata watendao uovu watakapo stawi, bado wataangamizwa kwenye uharibifu wa milele. 8 Lakini wewe, Yahwe, utatawala milele. 9 Hakika, watazame adui zako, Yahwe! Hakika, watazame adui zako. Wataangamia! Wale wote watendao maovu watatawanywa. 10 Wewe umeyainua mapembe yangu kama mapembe ya Nyati wa porini; nimepakwa mafuta safi. 11 Macho yangu yameona kuanguka kwa adui zangu; masikio yangu yamesikia maangamizi ya maadui zangu waovu. 12 Wenye haki watastawi kama mtende; watakua kama mwerezi wa Lebanoni. 13 Wamepandwa katika nyumba ya Yahwe; wakistawi katika nyua za Mungu wetu. 14 Wao huzaa matunda hata uzeeni; hukaa safi na wenye afya, 15 kutangaza kuwa Yahwe ni wa haki. Yeye ni mwamba wangu, na hakuna udhalimu ndani yake.

< Zaburi 92 >