< Zaburi 77 >

1 Nitampazia Mungu sauti yangu, nitamuita Mungu kwa sauti yangu, na Mungu wangu atanisikia. 2 Katika siku ya taabu nilimtafuta Bwana; usiku niliinua mikono yangu, nayo haikuchoka. Moyo wangu ulikataa kufarijiwa. 3 Ningali nikiugua nilielekeza mawazo yangu kwa Mungu. Nilimfikiria Mungu nilipokuwa dhaifu. (Selah) 4 Uliyafanya macho yangu yasisinzie; nilisumbuka sana kuongea. 5 Nilifikiri kuhusu siku za kale, kuhusu mambo yaliyopita muda mrefu. 6 Wakati wa usiku niliukumbuka wimbo niliouimba mara moja. Nilifikiria kwa makini na kujaribu kuelewa kile kilichokuwa kimetokea. 7 Je, Mungu atanikataa milele? Je, hatanionesha tena huruma? 8 Je, uaminifu wa agano lake ulikuwa umetoweka milele? Je, ahadi yake imeshindwa milele? 9 Je, Mungu amesahau kuwa mwenye neema? Je, hasira yake imeifunga huruma yake? (Selah) 10 Nilisema, “Hii ni huzuni yangu: mabadiliko ya mkono wa kuume wa Aliye Juu dhidi yetu.” 11 Lakini nitayakumbuka matendo yako, Yahwe; nitafikiri kuhusu matendo yako makuu yaliyopita. 12 Nitayatafakari matendo yako yote nami nitayaishi. 13 Njia yako, Mungu, ni takatifu; ni mungu gani wa kulinganishwa na Mungu wetu aliye mkuu? 14 Wewe ni Mungu utendaye maajabu; wewe umeonesha nguvu zako kati ya mataifa. 15 Uliwapa watu wako ushindi kwa uweza wako mkuu - ukoo wa Yakobo na Yusufu. (Selah) 16 Maji yalikuona wewe, Mungu; maji yalikuona wewe, nayo yakaogopa; vina vya maji vilitetemeka. 17 Mawingu yalitiririsha maji chini; anga zito lilitoa sauti; mishale yako ilipita kati. 18 Sauti yako kama ya radi ilisikika katika upepo; radi iliwasha dunia; nchi iliogopa na kutetemeka. 19 Njia yako ilipita baharini na mapito yako katika maji mengi, lakini alama za miguu yako hazikuonekana. 20 Uliwaongoza watu wako kama kundi kwa mkono wa Musa na Haruni.

< Zaburi 77 >