< Zaburi 71 >

1 Katika wewe, Yahwe, napatakimbilio salama; usiniache niaibishwe. 2 Uniokoe na kunifanya salama katika haki yako; geuzia sikio lako kwangu. 3 Uwe kwagu mwamba kwa ajili ya kimbilio salama ambako naweza kwenda siku zote; wewe umeamuru kuniokoa, kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu. 4 Uniokoe mimi, Mungu wangu, kutoka katika mkono wa asiye haki na katili. 5 Maana wewe ni tumaini langu, Bwana Yahwe. Nimekuamini wewe siku zote tangu nilipokuwa mtoto. 6 Nimekuwa nikisaidiwa na wewe tangu tumboni; wewe ndiye yule uliyenitoa tumboni mwa mama yangu; sifa zangu zitakuhusu wewe siku zote. 7 Mimi ni mfano bora kwa watu wangu; wewe ni kimbilio langu lenye nguvu. 8 Mama yangu atajawa na sifa zako, siku zote akikuheshimu. 9 Usinitupe katika siku za miaka ya uzee wangu; usiniache wakati nguvu zangu zitakapoisha. 10 Maana adui zangu wanazungumza kuhusu mimi; wale wanao fatilia uhai wangu wanapanga njama pamoja. 11 Wao husema, “Mungu amemuacha; mfuateni na mumchukue, maana hakuna yeyote awezaye kumuokoa yeye.” 12 Mungu, usiwe mbali nami; Mungu wangu, harakisha kunisaidia mimi. 13 Waaibishwe na kuharibiwa, wale walio adui wa uhai wangu; wavishwe laumu na kudharauliwa, wale watafutao kuniumiza. 14 Lakini nitakutumainia wewe siku zote na nitakusifu wewe zaidi na zaidi. 15 Kinywa changu kitaongea kuhusu haki yako na wokovu wako mchana kutwa, ingawa ziwezi kuzielewa maana ni nyingi mno. 16 Nitakuja na matendo yenye nguvu ya Bwana Yahwe; nitataja haki yako, yako pekee. 17 Mungu, tangu ujana wangu wewe umenifundisha; hata sasa ninatangaza matendo yako ya ajabu. 18 Hakika, hata niwapo mzee na mvi kichwani, Mungu, usiniache mimi, kama ambavyo nimekuwa nikitanga nguvu yako kwa vizazi vijavyo, na uweza wako kwa yeyote ajaye. 19 Pia haki yako, Mungu, iko juu sana; wewe ambaye umefanya mambo makuu, Mungu, ni nani aliye kama wewe? 20 Wewe ambaye umetuonesha sisi mateso mengi utatuhuisha tena na utatupandisha tena juu kutoka kwenye kina cha nchi. 21 Uiongeze heshima yangu; rudi tena na unifariji. 22 Nami pia nitakushukuru kwa kinubi kwa ajili ya uaminifu wako, Mungu wangu; kwako nitaimba sifa kwa kinubi, Mtakatifu wa Israel. 23 Midomo yangu itapiga kelele kwa sababu ya furaha wakati nikikuimbia sifa, hata kwa roho yangu, ambayo wewe umeikomboa. 24 Ulimi wangu pia utaongea kuhusu haki yangu mchana kutwa; maana wameaibishwa na kuvurugwa, wale waliotafuta kuniumiza.

< Zaburi 71 >