< Zaburi 59 >
1 Uniokoe dhidi ya adui zangu, Mungu wangu; uniweke mahali pa juu mbali na wale wanaoinuka dhidi yangu.
2 Uniweke salama mbali na wafanyao kazi ya uovu, na uniokoe dhidi ya watu wenye kiu ya damu.
3 Maana, tazama, wanasubiria uvamizini waniue. Wafanya maovu wenye nguvu hujikusanya wenyewe pamoja dhidi yangu, lakini sio kwa sababu ya makosa yangu au dhambi yangu, Yahwe.
4 Wao wanajiandaa kunikimbiza ingawa sina kosa; amka unisaidie na unitazame.
5 Ewe, Yahwe Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, inika uwaadhibu mataifa yote; usiwe na huruma kwa mhalifu mwovu yeyote. (Selah)
6 Wao wanarudi jioni, wanabweka kama mbwa na kuuzungukia mji.
7 Tazama, wanapiga kelele mbaya kwa midomo yao; panga ziko kwenye midomo yao, maana wanasema, “Ni nani anaye tusikia?”
8 Lakini wewe, Yahwe, utawacheka; wewe huwadhihaki mataifa yote.
9 Mungu, nguvu yangu, nitakuwa msikivu kwako; wewe ni mnara wangu mrefu.
10 Mungu atakutana nami akiwa na uaminifu wa agano lake; Mungu atanifanya nione shauku yangu juu ya adui zangu.
11 Usiwaue, hivyo watu watasahau. Uwatawanye kwa nguvu zako na uwaangushe, Bwana ngao yetu.
12 Kwa ajili ya dhambi za midomo yao na maneno ya midomo yao, wakamatwe katika majivuno yao, na kwa laana na uongo ambao wao huelezea.
13 Uwamalize katika gadhabu yako, uwamalize ili kwamba wasiwepo tena; wajue kuwa Mungu anatawala katika Yakobo na mwisho wa nchi. (Selah)
14 Wakati wa jioni wao hurudi, wakibweka kama mbwa wakiuzungukia mji.
15 Wanatangatanga wakitafuta chakula na wanabweka kama mbwa kama hawajatosheka.
16 Lakini nitaimba kuhusu nguvu zako, na asubuhi nitaimba kuhusu upendo wako imara! maana umekuwa mnara wangu mrefu na kimbilio la usalama katika siku ya taabu.
17 Kwako, nguvu yangu, nitaimba sifa; kwa kuwa Mungu ni mnara wangu mrefu, Mungu wa uaminifu wa agano.