< Zaburi 58 >

1 Je, ninyi watawala mnaongea haki? Mnahukumu kwa haki, ninyi watu? 2 Hapana, mnafanya uovu mioyoni mwenu; munaeneza vurugu nchi yote kwa mikono yenu. 3 Waovu huenenda katika upotovu hata walipokuwa tumboni; wao wanaenenda katika upotovu tangu kuzaliwa, wakiongea uongo. 4 Sumu yao ni kama sumu ya nyoka; wako kama fira kiziwi azibaye masikio yake, 5 ambaye hasikilizi sauti ya waganga, haijalishi ustadi walio nao. 6 Vunja meno yao midomoni mwao, Mungu; uyatoe meno ya mwana simba, Yahwe. 7 Wayeyuke kama maporomoko ya maji; wafyatuapo mishale yao, iwe kama haina ncha. 8 Wawe kama konokono ambaye huyeyuka na kutoweka, kama mtoto aliye zaliwa kabla ya wakati ambaye hakuona jua. 9 Kabla ya vyungu vyenu kupata joto la kuungua kwa miiba, yeye ataviondosha kwa upepo mkali, miiba ya kijani yote na ile inayoungua. 10 Mwenye haki atafurahia atakapoona kisasi cha Mungu; ataiosha miguu yake kwenye damu ya waovu, 11 hivyo watu watasema, “Hakika kuna tuzo kwa ajili ya mtu wenye haki; hakika kuna Mungu ahukumuye ulimwengu.”

< Zaburi 58 >