< Zaburi 35 >

1 Yahwe, uwashughulikie wale wanao nishughulikia mimi; upigane nao wanao pigana nami. 2 Uikamate ngao yako ndogo na ngao kubwa; inuka unisaidie. 3 Uutumie mkuki wako na shoka lako la vita kwa wale wanao nifukuzia; uuambie moyo wangu, “Mimi ni wokovu wako.” 4 Waaibishwe na kudharauliwa wale wanaoutafuta uhai wangu. Warudishwe nyuma na wafedheheshwe wanao panga kunidhuru. 5 Wao wawe makapi mbele ya upepo, malaika wakiwafutilia mbali. 6 Njia yao na iwe giza na utelezi, malaika wa Yahwe wakiwafukuzia. 7 Wamenitegea mtego bila sababu; bila sababu wamechimba shimo kwa ajili ya uhai wangu. 8 Uharibifu na uwapate wao kwa kushitukiza. Mtego ambao wameutega na uwanase wao. Na wadumbukie humo, ili kwamba waangamizwe. 9 Bali mimi nitakuwa nafuraha ndani ya Yahwe na ndani ya wokovu wake. 10 Mifupa yangu yote itasema, “Yahwe, ni nani kama wewe, uokoaye walio onewa mkononi mwa walio na nguvu kuwazidi wao na masikini na wahitaji mkononi mwa wale wanaojaribu kuwaibia?” 11 Mashahidi wa uongo wamesimama; wananishitakia uongo. 12 Kwa ajili ya wema wananilipa mabaya. Nina huzuni nyingi. 13 Lakini, walipokuwa akiugua, nilivaa magunia; nilifunga kwa ajili yao huku kichwa changu kikiinamia kifuani kwangu. 14 Nilienenda katika huzuni kana kwamba walikuwa ni ndugu zangu; niliinama chini nikiomboleza kana kwamba ni kwa ajili ya mama yangu. 15 Bali mimi nilipokuwa mashakani, walifurahi sana na kukutanika pamoja; walikutanika pamoja kinyume na mimi, nami nilishangazwa nao. Walinirarua bila kuacha. 16 Kwa dharau kabisa walinidhihaki; walinisagia meno yao. 17 Bwana, mpaka lini utaendelea kutazama? uiokoe roho yangu na mashambulizi yao ya maagamizi uyaokoe maisha yangu na simba. 18 Nami nitakushukuru wewe katika kusanyiko kubwa; nitakusifu kati ya watu wengi. 19 Usiwaache maadui zangu wadanganyifu kufurahi juu yangu; usiwaache waendelee na mipango yao ya uovu. 20 Kwa maana hawaongei amani, bali wanabuni maneno ya uongo kwa wale wanaoishi kwa amani katika ardhi yetu. 21 Midomo yao inapaza sauti ikinishtaki; wakisema, Aha, Aha, macho yetu yameona.” 22 Yahwe wewe umeona, usikae kimya; Bwana, usiwe mbali nami. 23 Inuka mwenyewe na usimame kunitetea; Mungu wangu na Bwana wangu, unitetee. 24 Kwa sabababu ya haki yako, Yahwe Mungu wangu, unitetee; usiwaache wafurahi kwa ajili yangu. 25 Usiwaache waseme mioyoni mwao, “Aha, tumepata tulicho kihitaji.” Usiwaache waseme, tumemmeza.” 26 Uwaaibishe na kuwa fendhehesha wale wanaotaka kunidhuru. Wale wote wanao ni dhihaki wafunikwe kwa aibu na kudharauliwa. 27 Nao wote wanao tamani kudhihirishwa kwangu washangilie na wafurahi; siku zote waseme, “Usifiwe Yahwe, yeye ajifurahishaye katika mafanikio ya mtumishi wake. 28 Kisha nitatangaza matendo yako ya haki na kukusifu wewe wakati wote.

< Zaburi 35 >