< Zaburi 3 >

1 Yahewh, maadui zangu wako wangapi! Ni wengi wamekuja kinyume na mimi. 2 Ni wengi wanaonisema, “Hakuna msaada wowote kutoka kwa Mungu kwa ajili yake.” (Selah) 3 Bali wewe, Yahweh, u ngao yangu pande zote, utukufu wangu, na uniinuaye kichwa changu. 4 Nampazia Yahweh sauti yangu, na yeye ananijibu kutoka katika mlima wake mtakatifu. 5 Nilijilaza chini na kusinzia; na niliamka, kwa kuwa Yahweh alinilinda. 6 Sitaogopa kusanyiko la watu ambao wamejipanga kinyume na mimi pande zote. 7 Inuka, Yahweh! Uniokoe, Mungu wangu! Kwa kuwa utawapiga maadui zangu wote kwenye taya zao; utayavunja meno ya waovu. 8 Wokovu unatoka kwa Yahweh. Baraka zako ziwe juu ya watu wako.

< Zaburi 3 >