< Zaburi 29 >

1 Mpeni sifa Yahwe, enyi wana wa Mungu! Mpeni sifa Yahwe kwa ajili ya utukufu wake na nguvu. 2 Mpeni Yahwe utukufu ambao jina lake linastahili. Mpigieni magoti Yahwe katika mapambo ya utakatifu. 3 Sauti ya Yahwe imesikika zaidi ya maji; Mungu wa radi ya utukufu, radi yaYahwe i juu ya maji mengi. 4 Sauti ya Yahwe ina nguvu; sauti ya Yahwe ni kuu. 5 Sauti ya Yahwe huivunja mierezi; Yahwe huivunja vipande vipande mierezi ya Lebanon. 6 Yeye huifanya Lebanoni kuruka kama ndama wa ng'ombe na Sirioni kama mwana wa nyati. 7 Sauti ya Yahwe hutoa miale ya moto. 8 Sauti ya Yahwe hutetemesha Jangwa; Yahwe hutetemesha jangwa la Kadeshi. 9 Sauti ya Yahwe huufanya miti mikubwa kutikisika na huipukutisha misitu. Kila mmoja katika hekalu lake husema, “Utukufu!” 10 Yahwe hukaa kama mfalme juu ya mafuriko; Yahwe hukaa kama mfalme milele. 11 Yahwe huwatia nguvu watu wake; Yahwe huwa bariki watu wake na amani.

< Zaburi 29 >