< Zaburi 2 >

1 Kwa nini mataifa wanafanya dhoruba, kwa nini watu wanafanya njama ambazo zitafeli? 2 Wafalme wa nchi kwa pamoja hushikilia misimamo yao na watawala kwa pamoja hufanya njama kinyume na Yahwe na kinyume na Masihi, wakisema, 3 “Ngoja tuzikate pingu walizo tufingia sisi na kuzitupa pingu zao.” 4 Yeye aketie katika mbingu atacheka kwa dharau mbele yao; Bwana atawadhihaki wao. 5 Kisha ataongea nao katika hasira yake na kuwaogofya kwa gadhabu yake, akisema, 6 “Mimi mwenyewe nilimpaka mafuta mfalme wa Sayuni, mlima wangu mtakatifu.” 7 Nami nitatangaza amri ya Yahwe. Yeye aliniambia, “wewe ni mwanangu! Leo hii nimekuwa baba yako. 8 Uniombe, nami nitakupa wewe taifa kwa ajili ya urithi na mikoa ya nchi iliyo bora kwa ajili ya umiliki wako. 9 Wewe utawavunja wao kwa fimbo ya chuma; kama vile mtungi wa mfinyanzi, wewe utawavunja wao vipande vipande.” 10 Hivyo sasa, ninyi wafalme; mchukue tahadhari; mjirekebishe. 11 Mwabuduni Yahwe kwa hofu na mfurahi mkitetemeka. 12 Mumbusu mwana vinginevyo atawakasirikia, na mtakufa pale pale hasira yake ikiwaka. Ni jinsi gani wamebarikiwa wale wote watafutao usalama ndani yake.

< Zaburi 2 >