< Zaburi 140 >

1 Yahwe, uniokoe dhidi ya waovu; unikinge dhidi ya watu wenye vurugu. 2 Wao wanapanga uovu mioyoni mwao; wanasababisha mapigano kila siku. 3 Ndimi zao zinajeruhi kama nyoka; sumu ya fira imo midomoni mwao. (Selah) 4 Ee Yahwe, unilinde dhidi ya mikono ya waovu; unikinge na vurugu za watu wanaopanga kuniangusha. 5 Wenye majivuno wameweka mtego kwa ajili yangu; wameeneza nyavu; wameweka kitanzi kwa ajili yangu. (Selah) 6 Nilimwambia Yahwe, “Wewe ni Mungu wangu; usikie kilio changu unihurumie.” 7 Ee Yahwe, Bwana wangu, wewe ni mwenye nguvu uwezaye kuniokoa; hunifunika ngao kichwa changu siku ya vita. 8 Ee Yahwe, usiyatimize matakwa ya waovu; usiruhusu njama zao kufanikiwa. (Selah) 9 Wale wanao nizunguka huinua vichwa vyao; madhara ya midomo yao wenyewe na yawafunike. 10 Makaa ya moto na yawaangukie; uwatupe motoni, kwenye shimo refu, wasiweze kuinuka tena. 11 Watu wenye ndimi na wasifanywe salama juu ya nchi; na uovu umuwinde kumpiga mtu mwenye vurugu mpaka afe. 12 Ninajua kuwa Yahwe atahukumu kwa haki walioteswa, na kuwa atawapa haki wahitaji. 13 Hakika watu wenye haki watalishukuru jina lako; watu wanyoofu wataishi uweponi mwako.

< Zaburi 140 >