< Zaburi 139 >

1 Ee Yahwe, wewe umenichunguza, na unanijua. 2 Wewe unajua nikaapo na niinukapo; unayajua mawazo yangu tokea mbali sana. 3 Unachunguza wenendo wangu na kulala kwangu; unazijua njia zangu zote. 4 Kabla hakujawa na neno kwenye ulimi wangu, wewe unalijua kabisa, Yahwe. 5 Nyuma yangu na mbele yangu unanizunguka na kuniwekea mkono wako. 6 Maarifa hayo ni mengi yananizidi mimi; yako juu sana, nami siwezi kuyafikia. 7 Niende wapi mbali na roho yako? Niende wapi niukimbie uwepo wako? 8 Kama nikipaa mbinguni, uko huko; kama nikifanya kitanda changu Kuzimuni, tazama, uko huko. (Sheol h7585) 9 Kama nikipaa kwa mbawa za asubuhi na kwenda kuishi pande za mwisho wa bahari, 10 hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika. 11 Kama nikisema, “Hakika giza litanifunika, na nuru inizungukayo itakuwa usiku,” 12 Hata giza lisingweza kuwa giza kwako. Usiku ungeng'aa kama mchana, maana giza na nuru kwako vinafanana. 13 Wewe uliumba sehemu zangu za ndani; uliniumba tumboni mwa mama yangu. 14 Nitakusifu, kwa maana nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu. Nafsi yangu yalijua hili vizuri sana. 15 Mifupa yangu haikusitirika kwako nilipoumbwa kwa siri, nilipoumbwa kwa ustadi pande za chini za nchi. 16 Uliniona ndani ya tumbo; siku zote zilizo pangwa kwangu ziliandikwa kitabuni mwako hata kabla ya siku ya kwanza kutokea. 17 Ni jinsi gani mawazo yako ni ya thamani kwangu, Mungu! Njinsi ilivyo kubwa jumla zake! 18 Kama nikijaribu kuyahesabu ni mengi kuliko mchanga. Niamkapo bado niko na wewe. 19 Ee Mungu, kama ungewaua waovu; ondokeni kwangu enyi watu wenye vurugu. 20 Wanakuasi wewe na kutenda udanganyifu; adui zako wananena uongo. 21 Je, siwachukii hao, wale wakuchukiao Yahwe? Je, siwadharau wale wanao inuka dhidi yako? 22 Nawachukia kabisa; wamekuwa adui zangu. 23 Ee Mungu, unichunguze na kuujua moyo wangu; unijaribu na uyajue mawazo yangu. 24 Uone kama kuna njia ya uovu ndani yangu, na uniongoze katika njia ya milele.

< Zaburi 139 >