< Zaburi 109 >

1 Zaburi ya Daudi. Mungu ninaye msifu, usinyamaze kimya. 2 Kwa maana waovu na wadanganyifu wananishambulia; wanazungumza uongo dhidi yangu. 3 Wananizunguka na kusema mambo ya chuki, na wananishambulia bila sababu. 4 Wananilipa kashfa badala ya upendo, lakini mimi ninawaombea. 5 Wananilipa uovu badala ya mema, na wanachukia upendo wangu. 6 Teua mtu mwovu aliye adui zaidi kama watu hawa; teua mshitaki asimame mkono wake wa kuume. 7 Na atakapohukumiwa, aonekane na hatia; maombi yake yachukuliwe kuwa ni dhambi. 8 Siku zake na ziwe chahe; mamlaka yake na yachukuliwe na mtu mwingine. 9 Watoto wake wawe yatima, na mke wake awe mjane. 10 Watoto wake wenye kutanga tanga na kuombaomba, wakiondoka katika nyumba zao zilizo haribika na kuomba chakula au pesa kwa wapita njia. 11 Mdai na achukue vitu vyake vyote amilikivyo; wageni wateke mapato ya kazi yake. 12 Asiwepo mtu yeyote wa kumfanyia wema; mtu yeyote asiwahurumie yatima wake. 13 Watoto wake waangamizwe; majina yao na yafutwe katika kizazi kijacho. 14 Uovu wa baba zake utajwe kwa Yahwe; na dhambi ya mama yake isisahaulike. 15 Hatia zao na ziwe mbele ya Yahwe siku zote; Yahwe na aiondoe kumbukumbu yao duniani. 16 Yahwe na afanye hivi kwa sababu mtu huyu kamwe hakusumbuka kuonesha uaminifu wa agano wowote, lakini badala yake aliwasumbua wanyonge, wahitaji, na kuwaua walio vunjika moyo. 17 Alipenda kulaani; na imrudie juu yake. Alichukia kubariki; baraka zozote na zisije kwake. 18 Alijivika kulaani kana kwamba ni vazi lake, na laana yake iliingia ndani yake kama maji, na kama mafuta mifupani mwake. 19 Laana zake na ziwe kwake kama vazi avaalo kujifunika mwenyewe, na kama mkanda avaao kila siku. 20 Na haya yawe malipo ya mshitaki wangu kutoka kwa Yahwe, ya wale wasemao mambo maovu juu yangu. 21 Yahwe Bwana wangu, unishughulikie kwa wema kwa ajili ya jina lako. Kwa sababu uaminifu wa agano lako ni mwema, uniokoe. 22 Kwa maana ni mnyonge na muhitaji, na moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu. 23 Ninatoweka kama kivuli cha jioni; ninapeperushwa kama nzige. 24 Magoti yangu ni dhaifu kutokana na kufunga; ninakuwa mwembamba na mifupa. 25 Nimedharauliwa na washitaki wangu; wanionapo; hutikisa vichwa vyao. 26 Nisaidie, Yahwe Mungu wangu; uniokoe kwa uaminifu wa agano lako. 27 Nao wajue kuwa wewe umefanya haya, kwamba wewe, Yahwe, umetenda haya. 28 Ingawa wananilaani, tafadhali unibariki; wanishambuliapo, waaibishwe, lakini mtumishi wako afurahi. 29 Washitaki wangu na wavishwe kwa aibu; wavae aibu yao kama vazi. 30 Kwa kinywa changu ninatoa shukrani kuu kwa Yahwe; nitamsifu yeye katikati ya kusanyiko. 31 Maana nitasimama mkono wa kuume wa mhitaji, ili nimuokoe dhidi ya wale wanao muhukumu.

< Zaburi 109 >