< Zaburi 104 >

1 Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote, Ewe Yahwe Mungu wangu, wewe ni mkubwa sana; umevikwa kwa utukufu na enzi. 2 Unajifunika mwenyewe kwa nuru kama kwa mavazi; umetandaza mbingu kama pazia za hema. 3 Umeweka mawinguni mihimili ya vyumba vyako; huyafanya mawingu gari lako; hutembea juu ya mbawa za upepo. 4 Yeye huufanya upepo kuwa wajumbe wake, miale ya moto kuwa watumishi wake. 5 Aliiweka misingi ya nchi, nayo haitahamishwa kamwe. 6 Wewe uliifunika nchi kwa maji kama kwa mavazi; maji yalifunika milima. 7 Kukemea kwako kulifanya maji kupungua; kwa sauti ya radi yako yakaondoka kasi. 8 Milima iliinuka, na mabonde yakaenea mahali ambapo wewe ulikwisha pachagua kwa ajili yao. 9 Umeweka mipaka kwa ajili yao ambao hayawezi kuupita; hayawezi kuifunika nchi tena. 10 Yeye alifanya chemchemi kutiririsha maji mabondeni; mito kutiririka katikati ya milima. 11 Inasambaza maji kwa ajili ya wanyama wote wa shambani; punda wa porini hukata kiu yao. 12 Kandokando ya mito ndege hujenga viota vyao; huimba kati ya matawi. 13 Humwagilia milima kutoka katika chumba chake cha maji mawinguni. Nchi imejazwa kwa matunda ya kazi yake. 14 Huzifanya nyasi kukua kwa ajili ya mifugo na mimea kwa ajili ya binadamu kulima ili kwamba mwanadamu aweze kuzalisha chakula toka nchini. 15 Hutengeneza mvinyo kumfurahisha mwanadamu, mafuta yakumfanya uso wake ung'ae, na chakula kwa ajili ya kuimarisha uhai wake. 16 Miti ya Yahwe hupata mvua nyingi; Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda. 17 Hapo ndege hutengeneza viota vyao. Na korongo, misunobari ni nyuma yake. 18 Mbuzi mwitu huishi kwenye milima mrefu; na urefu wa milima ni kimilio la wibari. 19 Aliuchagua mwezi kuweka alama ya majira; jua latambua kuchwa kwake. 20 Wewe hufanya giza la usiku ambapo wanyama wote wa msituni hutoka nje. 21 Wana simba huunguruma kwa ajili ya mawindo na hutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu. 22 Jua linapochomoza, huenda zao na kujilaza mapangoni mwao. 23 Wakati huo huo, watu hutoka nje kuelekea kazi zao na utumishi wake mpaka jioni. 24 Yahwe, ni jinsi gani kazi zako zilivyo nyingi na za aina mbalimbali! Kwa hekima ulizifanya zote; nchi inafurika kwa kazi zako. 25 Kule kuna bahari, yenye kina kirefu na pana, ikiwa na viume vingi visivyo hesabika, vyote vidogo na vikubwa. 26 Meli husafili humo, na ndimo alimo Lewiathani uliye muumba acheze baharini. 27 Hawa wote hukutazama wewe uwape chakula kwa wakati. 28 Unapowapa chakula, hukusanyika; ufunguapo mkono wako, wanatosheka. 29 Unapouficha uso wako, wanateseka; ukiiondoa pumzi yao, wanakufa na kurudi mavumbini. 30 Unapotuma Roho yako, wanaumbwa, nawe unaifanya upya nchi. 31 Utukufu wa Yahwe na udumu milele; Yahwe na aufurahie uumbaji wake. 32 Yeye hutazama nchi, nayo hutikisika; huigusa milima, nayo hutoa moshi. 33 Nitamwimbia Yahwe maisha yangu yote; nitamwimbia sifa Mungu wangu nigali ninaishi. 34 Mawazo yangu na yawe matamu kwake; nitafurahia katika Yahwe. 35 Wenye dhambi na waondoshwe katika nchi, na waovu wasiwepo tena. Ninamsifu Yahwe maisha yangu yote. Msifuni Yahwe.

< Zaburi 104 >