< Mithali 31 >
1 Maneno ya mfalme Lemueli - mausia aliyofundishwa na mama yake.
2 Mwanangu nini? Na ni nini mwana wa tumbo langu? Na ni nini mwana wa nadhiri zangu?
3 Nguvu zako usiwape wanawake; au wenye kuharibu wafalme njia zako.
4 Lemueli, kunywa divai, siyo kwa ajili ya wafalme, wala kwa watawala kuuliza, “kileo kikali kiko wapi?”
5 Kwa sababu kama watakunywa, watasahau sheria ni nini, na kupotosha haki za wote walioonewa.
6 Wape kileo kikali watu wanaopotea na mvinyo kwa wale wenye kutaabika kwa uchungu.
7 Atakunywa na kusahau umasikini wake na hataikumbuka taabu yake.
8 Ongea kwa ajili yao wasioweza kuongea, kwa madai ya wote wanaopotea.
9 Ongea na uhukumu kwa vipimo vya haki na utetee dai la masikini na watu wahitaji.
10 Mke hodari ni nani anaweza kumpata? Thamani yake ni zaidi kuliko vito.
11 Moyo wa mume wake humwamini, na hatakuwa masikini.
12 Humtendea mambo mema na wala si mabaya siku zote za maisha yake.
13 Huchagua sufu na kitani, na hufanya kazi yake ya mikono kwa furaha.
14 Yupo kama meli za wafanyabiashara; huleta chakula chake kutoka mbali.
15 Huamka wakati wa usiku na kuwapa chakula watu wa kaya yake, na kugawa kazi kwa watumishi wake wa kike.
16 Hulifikiria shamba na kulinunua, kwa tunda la mikono yake hupanda shamba la mizabibu.
17 Yeye mwenyewe hujivika nguvu na kuimarisha mikono yake.
18 Huangalia ni kipi kitaleta faida nzuri kwake; usiku wote taa yake haizimishwi.
19 Mikono yake huiweka kwenye mpini wa kisokotea nyuzi na hushikilia kisokotea nyuzi.
20 Mkono wake huwafikia watu masikini; mikono yake huwafikia watu wahitaji.
21 Haogopi theluji kwa ajili ya kaya yake, kwa maana nyumba yake yote imevika kwa nguo nyekundu.
22 Hutengeneza matandiko ya kitanda chake, na huvaa nguo za kitani ya dhambarau safi.
23 Mume wake anajulikana malangoni, anapoketi na wazee wa nchi.
24 Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza, na naleta mishipi kwa wafanyabiashara.
25 Amevaa nguvu na heshima, na wakati ujao huucheka.
26 Anafumbua kinywa chake kwa hekima na sheria ya ukarimu ipo kwenye ulimi wake.
27 Huangalia njia za nyumba yake na hawezi kula mkate wa uvivu.
28 Watoto wake huinuka na kumwita heri na mume wake humsifia, akisema,
29 “Wanawake wengi wamefanya vizuri, lakini wewe umewapita wote.”
30 Madaha ni udanganyifu, uzuri ni ubatili; bali mwanamke amchaye Yehova, atasifiwa.
31 Mpeni tunda la mikono yake na kazi zake zimsifu katika malango.