< Mithali 28 >

1 Waovu hukimbia wakati hakuna mtu anayewafukuza, bali wale watendao haki ni thabiti kama simba kijana. 2 Kwa sababu ya uhalifu wa nchi, kuna wakuu wengi, bali kwa mtu mwenye ufahamu na maarifa, itadumu kwa muda mrefu. 3 Mtu masikini mwenye kukandamiza watu wengine masikini ni kama mvua inayopiga ambayo haisazi chakula. 4 Wale wanaokataa sheria huwatukuza watu waovu, bali wale wenye kuitunza sheria hupigana dhidi yao. 5 Watu wabaya hawafahamu haki, bali wale wanaomtafuta Yehova wanafahamu kila kitu. 6 Ni bora mtu masikini ambaye anatembea katika uadilifu, kuliko mtu tajiri ambaye ni mdanganyifu katika njia zake. 7 Yeye anayetunza sheria ni mwana mwenye ufahamu, bali mwenye ushirika na walafi humwaibisha baba yake. 8 Anayepata mafanikio kwa kutoza riba kubwa anakusanya utajiri wake kwa ajili ya mwingine ambaye atakuwa na huruma kwa watu masikini. 9 Kama mtu atageuzia mbali sikio lake kusikia sheria, hata maombi yake ni chukizo. 10 Yeye anayempotosha mwenye uadilifu katika njia ya uovu ataangukia kwenye shimo lake mwenyewe, bali wakamilifu watapata urithi mwema. 11 Mtu tajiri anaweza kuwa mwenye hekima machoni pake mwenyewe, bali mtu masikini mwenye ufahamu atamtafuta. 12 Kunapokuwa na ushindi kwa wenye kutenda haki, kunafuraha kuu, bali wanapoinuka waovu, watu hujificha wenyewe. 13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali mwenye kutubu na kuziacha ataonyeshwa rehema. 14 Anafuraha ambaye huishi kwa unyenyekevu, bali anayeufanya moyo wake ataanguka katika taabu. 15 Kama simba anayeunguruma au dubu anayeshabulia ni kama mtawala mwovu juu ya watu masikini. 16 Mtawala anayekosa ufahamu ni mkandamizaji katili, bali mwenye kuchukia aibu atadumu katika siku zake. 17 Kama mtu anahatia kwa sababu amemwaga damu ya mtu, atakuwa mkimbizi hadi kifo na hakuna atakayemsaidia. 18 Mwenye kuenenda kwa ukaminifu atakuwa salama, bali mwenye njia ya udanganyifu ataanguka ghafla. 19 Anayefanya kazi kwenye shamba lake atapata chakula kingi, bali afuataye shughuli za upuuzi atapata umasikini mkubwa. 20 Mtu mwaminifu atapata baraka nyingi bali apataye utajiri wa haraka hawezi kukosa adhabu. 21 Siyo vema kuonyesha upendeleo, lakini kwa kipande cha mkate mtu atafanya ubaya. 22 Mtu mchoyo huharakisha kwenye utajiri, lakini hajui ni umasikini gani utakuja juu yake. 23 Anayemkaripia mtu baadaye atapata fadhila zaidi kutoka kwake kuliko mwenye kumsifia sana kwa ulimi wake. 24 Yule anayemwibia baba yake na mama yake na kusema, “Hiyo siyo dhambi,” ni mshirika wa mwenye kuharibu. 25 Mtu mwenye tamaa huchochea mafarakano, bali anayemtumaini Yehova atafanikiwa. 26 Yule anayeutumaini moyo wake mwenyewe ni mpumbavu, bali anayekwenda kwa hekima atajilinda mbali na hatari. 27 Mwenye kuwapa masikini hatapungukiwa kitu, bali anayewafumbia macho atapokea laana nyingi. 28 Watu waovu wanapoinuka, watu hujificha wenyewe, lakini watu waovu wataangamia, wale watendao haki wataongezeka.

< Mithali 28 >