< Mithali 23 >

1 Unapoketi kula pamoja na mtawala, angalia kwa uangalifu kilichopo mbele yako, 2 na kama ni mtu unayependa kula chakula sana weka kisu kooni. 3 Usitamani vinono vyake maana ni chakula cha uongo. 4 Usifanye kazi sana ili kupata mali; uwe na busara ya kutosha ili ujue wakati wa kuacha. 5 Je utaruhusu macho yako yaangaze juu yake? Itaondoka, maana itawaa mabawa kama tai na kuruka angani. 6 Usile chakula cha yule mwenye jicho baya- na usiwe na shauku ya vinono vyake, 7 maana ni mtu mwenye kuhesabu gharama ya chakula. “Kula na kunywa!” anakuambia, lakini moyo wake haupo pamoja nawe. 8 Utatapika kiasi kidogo ulichokula na utakuwa umepoteza sifa zako njema. 9 Usiongee katika usikivu wa mpumbavu, maana atadharau hekima ya maneno yako. 10 Usihamishe jiwe la mpaka wa kale au kunyang'anya mashamba ya yatima, 11 maana Mkombozi wao ni imara na atatetea kesi yao dhidi yako. 12 Elekeza moyo wako katika mafundisho na masikio yako kwenye maneno ya maarifa. 13 Usizuie kuadilisha mtoto, maana ukimchapa kwa fimbo, hatakufa. 14 Ni wewe unayepaswa kumchapa kwa fimbo na kuikoa nafsi yake kuzimu. (Sheol h7585) 15 Mwanangu, kama moyo wako una busara, basi moyo wangu utafurahi pia; 16 sehemu zangu ndani kabisa zitafurahi sana midomo yako inaponena haki. 17 Usiruhusu moyo wako kuwahusudu wenye dhambi, lakini endelea kumcha Yehova siku zote. 18 Hakika tumaini lako halitaondolewa na siku zako za hapo baadaye. 19 Sikia- wewe! - mwanangu, na uwe mwenye busara na uelekeze moyo wako katika njia. 20 Usishirikiane pamoja na walevi, au pamoja na walaji wa nyama walafi, 21 maana mlevi na mlafi wanakuwa masikini na usingizi utawavika kwa matambara. 22 Msikilize baba yako ambaye alikuzaa na usimdharau mama yako wakati akiwa mzee. 23 Inunue kweli, lakini usiiuze; nunua hekima, nidhamu, na ufahamu. 24 Baba yake mwenye haki atafurahia sana, na yule amzaaye mtoto mwenye busara atamfurahia. 25 Mfurahishe baba yako na mama yako na yule aliyekuzaa afurahie. 26 Mwanangu, nipe moyo wako na macho yako yachunguze njia zangu. 27 Maana malaya ni shimo refu, na mke wa mume mwingine ni kisima chembamba. 28 Anavizia kama mnyang'anyi na huongeza idadi ya wadanganyifu miongoni mwa wanadamu. 29 Nani mwenye taabu? Nani mwenye huzuni? Nani mwenye mapigano? Nani mwenye malalamiko? Nani mwenye majeraha bila sababu? Nani mwenye macho mekundu? 30 Ni wale ambao huzengea kwenye mvinyo, wale wanaojaribu kuchanganya mvinyo. 31 Usiutazame mvinyo ukiwa mwekundu, wakati unametameta kwenye kikombe na kutelemka kwa uraini. 32 Mwisho wake unauma kama nyoka na sumu yake kama kifutu. 33 Macho yako yataona vitu vigeni na moyo wako utatamka vitu vya ukaidi. 34 Utakuwa kama anayelala kwenye bahari au anayelala juu ya mlingoti. “ 35 Wamenipiga,” utasema, “lakini sikuumia. Wamenichapa, lakini sikuwa na hisia. Nitaamka lini? Nitatafuta kinywaji kingine.”

< Mithali 23 >