< Mithali 2 >

1 Mwanangu, kama ukiyapokea maneno yangu na kuzitunza amri zangu, 2 usikilize hekima na utaelekeza moyo wako katika ufahamu. 3 kama utalilia ufahamu na kupaza sauti yako kwa ajili ya ufahamu, 4 kama utautafuta kama fedha na kupekua ufahamu kama unatafuta hazina iliyojificha, 5 ndipo utakapofahamu hofu ya Yehova na utapata maarifa ya Mungu. 6 Kwa kuwa Yohova hutoa hekima, katika kinywa chake hutoka maarifa na ufahamu. 7 Yeye huhifadhi sauti ya hekima kwa wale wampendezao, yeye ni ngao kwa wale waendao katika uadilifu, 8 huongoza katika njia za haki na atalinda njia ya waaminifu kwake. 9 Ndipo utakapoelewa wema, haki, usawa na kila njia njema. 10 Maana hekima itaingia moyoni mwako na maarifa yataipendeza nafsi yako. 11 Busara itakulinda, ufahamu utakuongoza. 12 Vitakuokoa kutoka katika njia ya uovu, kutoka kwa wale waongeao mambo potovu. 13 Ambao huziacha njia za wema na kutembea katika njia za giza. 14 Hufurahia wanapotenda maovu na hupendezwa katika upotovu. 15 Hufuata njia za udanganyifu na kwa kutumia ghilba huficha mapito yao. 16 Busara na hekima zitakuokoa kutoka kwa mwanamke malaya, kutoka kwa mwanamke anayetafuta visa na mwenye maneno ya kubembeleza. 17 Yeye humwacha mwenzi wa ujana wake na kusahau agano la Mungu wake. 18 Maana nyumba yake huinama na kufa na mapito yake yatakupeleka kwa wale walioko kaburini. 19 Wote waiendeao njia yake hawatarudi tena na wala hawataziona njia za uzima. 20 kwa hiyo utatembea katika njia ya watu wema na kufuata njia za wale watendao mema. 21 Kwa wale watendao mema watafanya makazi yao katika nchi, na wale wenye uadilifu watadumu katika nchi. 22 Lakini waovu wataondolewa katika nchi na wale wasioamini wataondolewa katika nchi.

< Mithali 2 >