< Mithali 13 >

1 Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya baba yake, bali mwenye dhihaka hatasikiliza karipio. 2 Mtu hufurahia vitu vizuri kutokana na matunda ya kinywa chake, bali hamu ya wadanganyifu ni jeuri. 3 Yeye anayelinda kinywa chake huyalinda maisha, bali anayefumbua sana midomo yake atajiangamiza mwenyewe. 4 Hamu ya watu wavivu ni uchu lakini hawapati kitu, bali hamu ya watu wenye bidii hutoshelezwa sana. 5 Atendaye haki huchukia uongo, bali mtu mwovu hukinzana mwenyewe, na kufanya ya kuaibisha. 6 Wenye haki huwalinda wale ambao ni wakamilifu katika mapito yao, bali uovu huwaangusha wale watendao dhambi. 7 Kuna mtu ambaye hujitajirisha mwenyewe, lakini hana chochote na kuna mtu ambaye hutoa kila kitu, bado ni tajiri kweli. 8 Mtu tajiri anaweza kufidia maisha yake kwa mali zake, bali mtu masikini hatapokea kitisho cha aina hiyo. 9 Mwanga wa mtu atendaye haki hufurahia, bali taa ya waovu itazimika. 10 Kiburi huzaa mafarakano, bali kwa wale wasikiao shauri jema kuna hekima. 11 Penye majivuno mengi utajiri hufifia, bali yeye apataye pesa kwa kufanya kazi kwa mkono wake pesa zake zitaongezeka. 12 Tumaini linapoachwa, huvunja moyo, bali kukamilishwa kwa shauku ni mti wa uzima. 13 Yule ambaye anadharau fundisho bado atakuwa chini ya utawala wake, bali yeye ambaye anaheshimu amri atapewa thawabu. 14 Mafundisho ya mtu mwenye hekima ni chemchemi ya uzima, yanakuondoa kutoka kwenye mitego ya mauti. 15 Busara njema huleta fadhila, bali njia ya wadanganyifu haina mwisho. 16 Watu wenye busara hutenda kwa maarifa kwa kila uamuzi, bali mpumbavu huonyesha upuuzi wake. 17 Mjumbe mbaya huangukia kwenye shida, bali balozi mwaminifu huleta upatanisho. 18 Yeye ambaye hupuuza kurudiwa atapata umasikini na aibu, bali heshima itamjia yeye ambaye hujifunza kutokana na masahihisho. 19 Shauku iliyotambuliwa ni tamu kwa hamu, bali wapumbavu huchukia kuacha uovu. 20 Tembea pamoja na watu wenye hekima nawe utakuwa na hekima, bali rafiki wa wapumbavu atateseka. 21 Maafa huwakimbilia wenye dhambi, bali wale watendao haki hupewa thawabu kwa mema. 22 Mtu mwema huacha urithi kwa wajukuu wake, bali mali ya mwenye dhambi huwekwa akiba kwa yule atendaye haki. 23 Shamba la masikini lisilolimwa linaweza huzalisha chakula kingi, bali huchukuliwa kwa udhalimu. 24 Yeye ambaye hamrudi mwanawe humchukia, bali yule anayempenda mwanawe humjali kwa kumwadibisha. 25 Yeye atendaye haki hula hadi kutosheleza hamu yake bali tumbo la mwovu linanjaa daima.

< Mithali 13 >