< Mithali 11 >

1 Yehova huchukia vipimo ambavyo havipo sahihi, bali hufurahia uzani dhahiri. 2 Kinapokuja kiburi, ndipo aibu huja, bali unyenyekevu huleta hekima. 3 Uadilifu wa wenye haki huwaongoza, bali udanganyifu wa njia za wajanja utawaangamiza. 4 Utajiri hauna thamani siku ya ghadhabu, bali kwa kutenda haki hujilinda na mauti. 5 Mwenendo wa mtu mwema huinyosha njia yake, bali waovu wataanguka kwa sababu ya uovu wao. 6 Mwenendo mwema wa wale wampendezao Mungu utawalinda salama, bali wadanganyifu hunaswa katika shauku zao. 7 Mtu mwovu anapokufa, tumaini lake hupotea na tumaini lililokuwa katika nguvu zake linakuwa si kitu. 8 Yule atendaye haki hulindwa katika taabu na badala yake taabu humjia mwovu. 9 Kwa kinywa chake asiyeamini Mungu humwangamiza jirani yake, bali kwa maarifa wale watendao haki hulindwa salama. 10 Wanapofanikiwa watendao haki, mji hufurahi, waovu wanapoangamia, kunakuwa na kelele za furaha. 11 Kwa zawadi nzuri za wale wanaompendeza Mungu, mji unakuwa mkubwa; kwa kinywa cha waovu mji huvurugwa. 12 Mtu mwenye dharau kwa rafiki yake hana akili, bali mtu mwenye ufahamu hunyamaza. 13 Anayekwenda akizunguka kwa kukashifu hufunua siri, bali mtu mwaminifu hustiri jambo. 14 Pasipokuwa na uongozi wenye busara, taifa huanguka, bali ushindi huja kwa kushauriana washauri wengi. 15 Anayemdhamini mkopo wa mgeni ataumia kwa usumbufu, bali anayechukia kutoa rehani kwa namna ya ahadi yupo salama. 16 Mwanamke mwenye rehema hupata heshima, bali watu wakorofi hufumbata utajiri. 17 Mtu mkarimu hufaidika mwenyewe, bali mkatili hujiumiza mwenyewe. 18 Mtu mwovu husema uongo kupata mishahara yake, bali yeye apandaye haki anavuna mishahara ya kweli. 19 Mtu mwaminifu atendaye haki ataishi, bali yeye atendaye uovu atakufa. 20 Yehova anawachukia wenye ukaidi mioyoni, bali anawapenda wale ambao njia zao hazina makosa. 21 Uwe na uhakika juu ya hili- watu waovu hawatakosa adhabu, bali uzao wa wale watendao haki watawekwa salama. 22 Kama pete ya dhahabu kwenye pua ya nguruwe ndiyo alivyo mwanamke mzuri asiye na busara. 23 Shauku ya wale watendao haki ni matokeo mema, bali watu waovu wanaweza kutumainia ghadhabu tu. 24 Kuna yule ambaye hupanda mbegu- atakusanya zaidi; mwingine hapandi- huyo anakuwa masikini. 25 Mtu mkarimu atafanikiwa na yule awapaye maji wengine atapata maji yake mwenyewe. 26 Watu wanamlaani mtu ambaye hukataa kuuza nafaka, bali zawadi njema hufunika kichwa chake ambaye huuza nafaka. 27 Yule ambaye hutafuta mema kwa bidii pia anatafuta kibali, bali yule atafutaye ubaya atapata ubaya. 28 Wale wanaotumaini utajiri wataanguka, bali kama jani, wale watendao haki watasitawi. 29 Yule ambaye analeta taabu kwenye kaya yake ataurithi upepo na mpumbavu atakuwa mtumishi wa wenye moyo wa hekima. 30 Wale watendao haki watakuwa kama mti wa uzima, lakini vurugu huondoa uzima. 31 Tazama! Ikiwa wale watendao haki hupokea wanachositahili, je si zaidi kwa waovu na wenye dhambi!

< Mithali 11 >