< Hesabu 23 >

1 Balaamu akamwabia Balaki, “Jenga madhabahu saba kwa ajili yangu na uandae mafahari saba na kondoo dume saba.” 2 Kwa hiyo Balaki akafanya kama Balaamu alivyoomba. Kisha Balaki na Balaamu wakatoa sadaka ya fahari mmoja na kondoo dume mmoja kwa kila madhabahu. 3 Ndipo Balaamu alipomwamiba Balaki, “Simama kwenye sadaka yako ya kuteketezwa na mimi nitaenda. Labda BWANA atakuja kukutana na mimi. Chochote atakachoniambia nitakuambia.” Kwa hiyo akaenda juu ya mlima usiokuwa na miti. 4 Wakati bado akiwa juu ya mlima. Mungu akakutana naye, na Balaamu akamwambia, “Nimejenga madhabahu saba, na nimetoa sadaka ya fahari na kondoo dume kwa kila madhabahu.” 5 BWANA akaweka ujumbe kwenye kinywa cha Baalamu akasema, “Rudi kwa Balaki ukamwambie.” 6 Kwa hiyo Balaamu akarudi kwa Balaki aliyekuwa amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, na viongozi wote wa Moabu walikuwa pamoja naye. 7 Ndipo Balaamu alipoanza kunena unabii wake akisema, “Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka katika milima ya mashariki, 'Njoo, nilaanie Yakobo kwa ajili yangu,' alisema, 'Njoo umtie unajisi Israeli,' 8 Nawezaje kuwalaani wale ambao Mungu hajawalaani? Nawezaje kuwapinga wale ambao Mungu hawapingi? 9 Kwa kuwa kutoka juu ya miamba Ninamwona; kutoka kwenye milima ninamtazama. Kuna watu wanaoishi pekee yao na hawajioni wenyewe kama ni taifa la kawaida. 10 Nani awezaye kuyahesabu mavumbi ya Yakobo au kuhesabu hata robo ya Israeli? Naomba nife kifo cha mtu mwenye haki, na mwisho wa maisha yangu uwe kama wake!” 11 Balaki akamwambia Balaamu, “Umenifanyia nini? Nilikuleta ili uwalaani maadui wangu, lakini ona, umewabariki,” 12 Balaamu akajibu akasema, “Kwa nini nisiwe mwangalifu kusema kile ambacho BWANA anaweka kinywani mwangu?” 13 Basi Balaki akamwambia, “Hebu uje nami kwenye eneo jingine ili uwaone. Utakaowaona ni wale wa karibu tu, huwezi kuwaona wote. Huko sasa unaweza kunilaania hawa watu.” 14 Kwa hiyo akampeleka Balaamu kwenye shamba la Zofimu, lililo juu ya Mlima Pisiga, na kule akajenga madhabau zingine saba. Akatoa sadaka ya fahari mmoja na kondoo dume kwa kila madhabahu. 15 Kisha Balaamu akamwambia Balaki, “Simama hapa karibu na sadaka zako, wakati mimi naenda kukutana na BWANA kule.” 16 Kwa hiyo BWANA akakutana na Balaamu na kumwekea ujumbe kinywani mwake. Alimwambia, “Rudi kwa Balaki ukamwambie huu ujumbe toka kwangu.” 17 Balaamu akamrudia, na tazama, alikuwa amesimama karibu na sadaka zake za kuteketezwa, na vionigozi wa Moabu walikuwa pamoja naye. Balaki akamwuliza, “BWANA amekwambiaje?” 18 Balaamu akaanza kutoa unabii. Akasema, “Inuka, Balaki na usikilize. Nisikilize mimi wewe mwana wa Zippori. 19 Mungu siyo mtu, kwamba umdanganye, au mwanadamu awezaye kubadili mawazo. Je, alishawahi kuahidi kitu pasipo kukitekeleza? Je, alishawahi kusema kuwa atafanya kitu bila kufanya kama alivyosema? 20 Tazama, Mimi nimeamriwa kuwabariki. Mungu ametoa baraka, nami siwezi kuibadilisha. 21 Hajawahi kuona magumu katika Yakobo au tabu katika Israeli. BWANA Mungu wao yuko pamoja nao, na kelele za wafalme wao ziko pamoja nao. 22 Mungu aliwatoa Misri kwa nguvu kama za nyati. 23 Hakuna uganga utakaofanikiwa dhidi ya Yakobo, na hakuna uchawi utakaomwumiza Israeli. Badala yake, itasemwa juu ya Yakobo na Israeli, 'Tazama kile ambacho Mungu amefanya!' 24 Tazama, watu wanainuka kama simba jike, kama vile simba ainukavyo na kuvamia. Halali chini mpaka ale windo lake na kunywa damu ya windo lake,” 25 Kisha Balaki akamwambia Balaamu, “Kamwe usiwalaani wala kuwabariki.” 26 Lakini Balaamu akamjibu Balaki, “Sijakuambia kuwa nitasema yote ambayo BWANA ananiambia kusema? 27 Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo sasa, Nami nitakupeleka mahali pengine. Labda kule itampendeza Mungu kunilaania hawa hawa watu.” 28 Kwa hiyo Balaki akampeleka Balaamu juu ya Mlima Peori, ambao unalitazama chini lile jangwa, 29 Balaamu akamwambia Balaki, “Nijengee madhabahu saba hapa na uniandalie mafahari saba na kondoo duume saba. 30 “Kwa hiyo Balaki akafanya kama alivyoambiwa; akatoa sadaka ya fahari na kondoo mume kwenye kila madhabahu.

< Hesabu 23 >