< Nahumu 3 >

1 Ole kwa mji uliojaa damu! Wote umejaa uongo na mali za wizi; wahanga wapo kwake daima. 2 Lakini sasa kunasauti ya mijeledi na sauti za kugongesha matairi, farasi wakicheza, na magari ya vita yanaruka ruka. 3 Kuna wapanda farasi wanashambulia, Upanga unang'ara, mikuki inametameta, marundo ya maiti, mafungu makubwa ya miili; hakuna ukomo wa miili, washambuliaji wanajikwaa juu yake. 4 Hii inatokea kwa sababu ya matendo ya tamaa ya kahaba mzuri, mzoefu wa uchawi, mwenye kuuza taifa kwa umalaya wake, na watu kwa njia ya matendo yake ya kichawi. 5 “Tazama, mimi nipo kinyume na wewe- hili ni neno la Yehova wa majeshi- sketi yako nitaiinua juu ya uso wako na kuzionyesha sehemu zako za siri kwa mataifa, aibu yako kwa falme. 6 Nitarusha uchafu wa kuchukiza na kukufanya uwe mbaya sana; nitakufanya uwe mtu wa kutazamwa na kila mmoja. 7 Itakuwa kwamba kila mmoja anayekutazama atakukimbia na kusema, “Ninawi ameharibika; ni nani ataomboleza kwa ajili yake?' Ni wapi nitampata mtu anayeweza kukufariji?” 8 Ninawi, je wewe ni bora kuliko Noamoni, uliojengwa juu ya Mto Naili, uliokuwa umezungukwa na maji, ambao ulinzi wake ilikuwa bahari, ambao ukuta wake ilikuwa bahari yenyewe? 9 Ethiopia na Misri zilikuwa nguvu zake, na mwisho wake haukuwepo; Putu na Libya walikuwa rafiki zake. 10 Lakini Noamoni alichukuliwa; alikwenda kwenye mateka; watoto wake wadogo walivunjwa vipande vipande katika kila makao makuu ya mtaa; adui zake walipiga kura kwa watu wake wenye heshima na wakuu wake wote walifungwa minyororo. 11 Wewe pia utalewa; utajaribu kujificha, na utatafuta makimbilio kutoka kwa adui yako. 12 Ngome zako zote zitakuwa kama mitini yenye tini zilizoiva mapema: kama zikitikiswa, zitaangukia kwenye kimywa cha mlaji. 13 Tazama, watu miongoni mwenu ni wanawake; malango ya nchi yako yamefunguliwa sana kwa ajili ya adui zako; moto umeharibu bawaba zake. 14 Nenda ukachote maji kwenye boma iliyozingirwa; ziimarishe ngome zako; nenda kwenye udongo na kandamiza matope; finyanga kwa ajili ya matofali. 15 Moto utakuteketeza pale, na upanga utakuangamiza. Utateketezwa kama nzige wachanga wanavyoteketeza kila kitu. Ninyi wenyewe mjitengeneze kuwa wengi kama nzige wachanga, na wengi kama nzinge waliopevuka. 16 Umezidisha wafanyabiashara wako zaidi kuliko nyota mbinguni; lakini wapo kama tunutu: wanapora nchi na kisha kuruka kwenda mbali. 17 Wafalme wenu wapo wengi kama zinge, na wakuu wenu wa majeshi ni kama kundi la wadudu wenye kuweka kambi katika ukuta wakati wa baridi. Lakini jua linapowaka wanaruka kwenda mbali ambako hakuna anayepajua. 18 Mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wamelala; watawala wako wamejilaza chini kupumzika. Watu wako wametawanyika juu ya milima, na hakuna hata mmoja wa kuwakusanya. 19 Hakuna uponyaji unaowezekana kwa ajili ya vidonda vyako. Vidonda vyako ni vikubwa. Wanaosikia habari juu yako watapiga makofi kwa furaha juu yako. Ni nani aliyejiepusha kwa uovu wako wa daima?

< Nahumu 3 >