< Mathayo 7 >

1 Usihukumu, nawe usije ukahukumiwa. 2 Kwa hukumu unayohukumu, nawe utahukumiwa. Na kwa kipimo unachopima na wewe pia utapimiwa hicho hicho. 3 Na kwa nini unatazama kipande cha mti kilichoko kwenye jicho la ndugu yako, lakini hutambuwi kipande cha gogo ambalo limo katika jicho lako? 4 Unawezaje kusema kwa ndugu yako, ngoja nikutolee kipande kilichomo kwenye jicho lako, wakati kipande cha gogo kimo ndani ya jicho lako? 5 Mnafiki wewe; kwanza toa gogo lililomo kwenye jicho lako, na ndipo utakapoweza kuona vizuri na kukitoa kipande cha mti kilichomo kwenye jicho la ndugu yako. 6 Usiwape mbwa kilicho kitakatifu, na usiwarushie nguruwe lulu mbele yao. Vinginevyo wataviharibu na kuvikanyaga kwa miguu, na tena watakugeukia wewe na kukurarua vipande vipande. 7 Omba, nawe utapewa. Tafuta, nawe utapata. Bisha hodi, na wewe utafunguliwa. 8 Kwa yeyote anayeomba, hupokea. Na kwa yeyote anayetafuta, hupata. Na kwa mtu ambaye anayebisha hodi, atafunguliwa. 9 Au kuna mtu miongoni mwenu ambaye, ikiwa mtoto wake amemwomba kipande cha mkate atampa jiwe? 10 Au ikiwa atamwomba samaki, na yeye atampa nyoka? 11 Kwa hiyo, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu zawadi nzuri, Je! Ni kiasi gani zaidi Baba aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wanao muomba yeye? 12 Kwa sababu hiyo, unapotaka kufanyiwa kitu chochote na watu wengine, nawe pia itakupasa kuwafanyia hivyo hivyo wao. Kwa kuwa hiyo ni sheria na manabii. 13 Ingieni kwa kupitia geti jembamba. Kwa kuwa geti ni pana na njia ni pana inayoongoza kwenye uharibifu, na kuna watu wengi wanaopitia njia hiyo. 14 Geti ni jembamba, Geti jembamba ni njia inayongooza katika uzima na ni wachache wanaoweza kuiona. 15 Jihadhari na manabii wa uongo, wanaokuja wamevaa ngozi ya kondoo, lakini kweli ni mbweha wakali. 16 Kwa matunda yao mtawatambua. Je watu wanaweza kuvuna matunda kwenye miba, au mtini kwenye mbengu ya mbaruti? 17 Kwa jinsi hiyo, kila mti mzuri huzaa matunda mazuri, lakini mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 Kila mti ambao hauzai matunda mazuri utakatwa na kutupwa katika moto. 20 Hivyo basi, utawatambua kutokana na matunda yao. 21 Si kila mtu aniambiaye mimi, 'Bwana, Bwana,' ataingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yule pekee atendaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 Watu wengi wataniambia siku hiyo, 'Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, hatukutoa mapepo kwa jina lako, na kwa jina lako tulifanya matendo mengi makuu?' 23 Ndipo nitawaambia wazi, 'sikuwatambua ninyi! Ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu!' 24 Kwa hiyo, kila mmoja asikiaye maneno yangu na kutii atafanana na mtu mwenye hekima aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. 25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukaja na ukaipiga nyumba hiyo, lakini haikuweza kuanguka chini, kwa kuwa ilikuwa imejengwa juu ya mwamba. 26 Lakini kila mtu anayesikia neno langu na asilitii, atafananishwa na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. 27 Mvua ikaja, mafuriko yakaja, na upepo ukaja na kuipiga nyumba hiyo. Na ikaanguka, na uharibifu wake ukakamilika.” 28 Ulifika wakati ambao Yesu alipomaliza kuongea maneno haya, makutano walishangazwa na mafundisho yake, 29 kwa kuwa alifundisha kama mtu mwenye mamlaka, na si kama waandishi wao.

< Mathayo 7 >