< Mathayo 15 >
1 Ndipo Mafarisayo na waadishi walikuja kwa Yesu kutoka Yerusalemu. Na kusema,
2 “Kwa nini wanafunzi wanayahalifu mapokeo ya wazee? Kwa kuwa hawanawi mikono yao wanapokuwa wanakula chakula.''
3 Yesu akawajibu na kuwaambia, “Nanyi kwa nini mnaihalifu sheria ya Bwana kwa ajili ya mapokeo yenu?
4 Kwa kuwa Mungu alisema, 'Mheshimu baba yako na mama yako; na 'Asemaye uovu kwa baba yake na mama yake, hakika atakufa.'
5 Lakini ninyi husema, 'Kila amwambiaye baba yake na mama yake, '“Kila msaada ambao angepata kutoka kwangu sasa ni zawadi kutoka kwa Mungu,'''
6 “Mtu huyo hana haja ya kumuheshimu baba yake. Katika namna hii mmelitangua neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu.
7 Enyi wanafiki, ni vema kama Isaya alivyo tabiri juu yenu aliposema,
8 'Watu hawa wananiheshimu mimi kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami.
9 Wananiabudu bure, kwa sababu wanafundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu.”'
10 Ndipo akawaita makutano na kuwaambia,” Sikilizeni na mfahamu
11 Hakuna kitu kiingiacho mdomoni mwa mtu na kumfanya najisi. Bali, kile kitokacho kinywani, hiki ndicho kimfanyacho mtu kuwa najisi.''
12 Ndipo wanafunzi wakamwendea na kusema na Yesu, “Je!, Unafahamu Mafarisayo walipolisikia lile neno walikwazika?”
13 Yesu aliwajibu na kusema, “Kila mmea ambao Baba yangu wa mbinguni hajaupanda utang'olewa.
14 Waacheni pekee, wao ni viongozi vipofu. Kama mtu kipofu atamuongoza kipofu mwenzake, wote wawili wataanguka shimoni.”
15 Petro akajibu na kumwambia Yesu,” Tuelezee mfano huu kwetu,
16 Yesu akajibu, ''Nanyi pia bado hamuelewi?
17 Ninyi hamuoni kuwa kila kiendacho mdomoni hupitia tumboni na kwenda chooni?
18 Lakini vitu vyote vitokavyo mdomoni hutoka ndani ya moyo. Ndivyo vitu vimtiavyo mtu unajisi.
19 Kwa kuwa katika moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushuhuda wa uongo, na matusi.
20 Haya ndiyo mambo yamtiayo mtu unajisi. Lakini kula bila kunawa mikono hakumfanyi mtu kuwa najisi.”
21 Ndipo Yesu akatoka mahali pale na akajitenga kuelekea pande za miji ya Tiro na Sidoni.
22 Tazama akaja mwanamke Mkanani kutoka pande hizo. Akapaza sauti akisema, ''Nihurumie, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu anateswa sana na pepo.''
23 Lakini Yesu hakumjibu neno. Wanafunzi wake wakaja wakimsihi, wakisema, ''Muondoe aende zake, maana anatupigia kelele.''
24 Yesu aliwajibu na kusema, Sikutumwa kwa mtu yeyoye isipokuwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.''
25 Lakini alikuja na kuinama mbele yake, akisema, ''Bwana nisaidie.''
26 Alimjibu na kusema, “Siyo vema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa,”
27 Akasema, “Ndiyo, Bwana, hata hivyo mbwa wadogo hula chakula kiagukacho mezani mwa Bwana wao.”
28 Ndipo Yesu akajibu na akisema “Mwanamke, imani yako ni kubwa. Na ifanyike kwako kama utakavyo.” Na binti yake alikuwa ameponywa katika wakati huo.
29 Yesu aliondoka mahali pale na kwenda karibu na bahari ya Galilaya. Kisha alienda juu ya mlima na kuketi huko.
30 Kundi kubwa likaja kwake. Na kumletea viwete, vipofu, bubu, vilema na wengine wengi, waliokuwa wagonjwa. Waliwaweka katika miguu ya Yesu na akawaponya.
31 Nao umati wakashangaa walipoona mabubu wakiongea, na vilema wakifanywa wazima, viwete wakitembea, na vipofu wakiona. Walimsifu Mungu wa Israeli.
32 Yesu akawaita wanafunzi wake na kusema, “Nimewaonea huruma umati, kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu bila kula kitu chochote. Sitawaaga waende kwao bila kula, wasije wakazimia njiani.”
33 Wanafunzi wake wakamwambia, “Ni wapi tunaweza kupata mikate ya kutosha hapa nyikani kushibisha umati mkuwbwa hivi?”
34 Yesu akawaambia, “Mna mikate mingapi?” Wakasema, “Saba, na samaki wadogo wachache.”
35 Yesu akawaamuru umati uketi chini.
36 Aliitwaa ile mikate saba na samaki, na baada ya kushukuru, akaimega na kuwapa wanafunzi. Wanafunzi wakawapa umati.
37 Watu wote wakala na kutosheka. Na wakakusanya mabaki ya vipande vya chakula vilivyosalia vipande vipande, vilijaa vikapu saba.
38 Wote waliokula walikuwa wanaume elfu nne bila wanawake na watoto.
39 Kisha Yesu akauaga umati waende zao na akaingia ndani ya mashua na kwenda sehemu za Magadani.