< Marko 13 >

1 Yesu alipokuwa akitembea kutoka hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake akamwuliza, “Mwalimu, tazama mawe haya yakushangaza na majengo!”
Yesu alipokuwa akitoka Hekaluni, mmojawapo wa wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu! Tazama jinsi mawe haya yalivyo makubwa, na majengo haya yalivyo mazuri!”
2 Akamwambia, Unaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalo salia juu ya jingine ambalo halitaangushwa chini”.
Ndipo Yesu akajibu akasema, “Je, unayaona majengo haya yalivyo makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali yote yatabomolewa.”
3 Naye alipokuwa amekaa juu ya Mlima wa Mizeituni nyuma ya hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamwuliza kwa siri,
Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni mkabala na Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamuuliza faraghani,
4 “Tuambie, mambo haya yatakuwa lini? Ni nini dalili ya mambo haya kutokea?”
“Tafadhali tuambie, mambo haya yatatukia lini? Nayo dalili ya kuwa hayo yote yanakaribia kutimia itakuwa gani?”
5 Yesu alianza kuwaambia, “Kuweni makini kwamba mtu yoyote asiwapotoshe.
Yesu akawaambia: “Jihadharini mtu yeyote asiwadanganye.
6 Wengi watakuja kwa jina langu wakisema, 'Mimi ndiye', na watawapotosha wengi.
Wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye,’ nao watawadanganya wengi.
7 Mtakaposikia vita na tetesi za vita, msiogope; mambo haya hayana budi kutokea, lakini mwisho bado.
Msikiapo habari za vita na uvumi wa vita, msiwe na hofu. Mambo haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.
8 Taifa litainuka kinyume na taifa jingine, na ufalme kinyume na ufalme. Patakuwa na matetemeko sehemu mbalimbali, na njaa. Huu ni mwanzo wa utungu.
Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na mitetemeko sehemu mbalimbali na njaa. Haya yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.
9 Iweni macho. Watawapeleka hadi mabarazani, na mtapingwa katika masinagogi. Mtasimamishwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, kama ushuhuda kwao.
“Lakini ninyi jihadharini. Kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kupigwa mijeledi katika masinagogi. Mtashtakiwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao.
10 Lakini injili lazima kwanza ihubiriwe kwa mataifa yote.
Nayo habari njema lazima ihubiriwe kwanza kwa mataifa yote kabla ule mwisho haujawadia.
11 Watakapo wakamata na kuwakabidhi, msiogope kuhusu kile mtakachosema. Ndani ya muda huo, mtapewa nini cha kusema; hamtakuwa ninyi mtakaoongea, bali Roho Mtakatifu.
Mtakapokamatwa na kushtakiwa, msisumbuke awali kuhusu mtakalosema. Semeni tu lolote mtakalopewa wakati huo, kwa kuwa si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho Mtakatifu.
12 Ndugu atamshitaki ndugu kuuawa, baba na mtoto wake. Watoto watasimama kinyume cha baba zao na kuwasababisha kuuawa.
“Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe.
13 Mtachukiwa na kila mtu kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, mtu huyo ataokoka.
Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
14 Mtakapoona chukizo la uharibifu limesimama pale lisipotakiwa kusimama (asomaye na afahamu), ndipo walioko ndani ya Yuda wakimbilie milimani,
“Mtakapoona ‘chukizo la uharibifu’ limesimama mahali pasipolipasa (asomaye na afahamu), basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani.
15 naye aliyeko juu ya nyumba asishuke chini ya nyumba, au kuchukua chochote kilichoko nje,
Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke au kuingia ndani ili kuchukua chochote.
16 na aliyeko shambani asirudi kuchukua vazi lake.
Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.
17 Lakini ole wao wanawake wenye mimba na wanyonyeshao katika siku hizo!
Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!
18 Ombeni kwamba isitokee wakati wa baridi.
Ombeni mambo haya yasitokee wakati wa baridi.
19 Kwani patakuwa na mateso makubwa, ambayo hayajawahi kutokea, tangu Mungu alipoumba ulimwengu, mpaka sasa, hapana, wala haitatokea tena.
Kwa maana siku hizo zitakuwa za dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo, hapo Mungu alipoumba ulimwengu, mpaka leo, na wala haitakuwako tena kamwe.
20 Mpaka Bwana atakapopunguza siku, hakuna mwili utakaookoka, lakini kwa ajili ya wateule, atakaowachagua, atapunguza namba za siku.
Kama Bwana asingelifupisha siku hizo, kamwe asingeliokoka mtu yeyote. Lakini kwa ajili ya wateule, wale aliowachagua, amezifupisha siku hizo.
21 Wakati huo kama mtu yeyote atawaambia, Tazama, Kristo yuko hapa!' au 'Tazama, yuko pale!' msiamini.
Wakati huo mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristohuyu hapa!’ au, ‘Tazama, yuko kule,’ msisadiki.
22 Kwani Wakristo wa uongo na manabii wa uongo watatokea na watatoa ishara na maajabu, ili kwamba, wawadanganye, yamkini hata wateule.
Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara na maajabu ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule.
23 Iweni macho! Nimekwisha wambia haya yote kabla ya wakati.
Hivyo jihadharini. Nimekwisha kuwaambia mambo haya yote mapema kabla hayajatukia.
24 Lakini baada ya mateso ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga wake,
“Lakini katika siku hizo, baada ya hiyo dhiki, “‘jua litatiwa giza nao mwezi hautatoa nuru yake;
25 nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu zilizoko mbinguni zitatikisika.
nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’
26 Ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu kubwa na utukufu.
“Ndipo watu wote watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu.
27 Ndipo atatuma malaika zake na atawakusanya pamoja wateule wake kutoka pande kuu nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.
Naye atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka miisho ya dunia hadi miisho ya mbingu.
28 Kwa mtini jifunzeni. Kama tawi liwezavyo kutoa na kuweka haraka majani yake, ndipo mtajua kwamba kiangazi kiko karibu.
“Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
29 Ndivyo ilivyo, mtakapoona mambo haya yakitokea, jueni kwamba yuko karibu, na malango.
Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yakitukia, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni.
30 Kweli, nawambieni, hiki kizazi hakitapita mbali kabla mambo haya hayajatokea.
Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.
31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
32 Lakini kuhusu siku hiyo au saa, hakuna ajuaye, hata malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba.
“Kwa habari ya siku ile na saa hakuna yeyote ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.
33 Iweni macho, Tazama, kwa sababu hamjui ni muda gani yatatokea. (Zingatia: Mstari huu, “Muwe waangalifu, Tazameni na ombeni kwa sababu...” haumo kwenye nakala za kale).
Jihadharini! Kesheni! Kwa maana hamjui wakati ule utakapowadia.
34 Ni kama mtu anayeenda safarini: akaacha nyumba yake, na kumweka mtumwa wake kuwa mtawala wa nyumba, kila mmoja na kazi yake. Na kumwamuru mlinzi kukaa macho.
Ni kama mtu anayesafiri. Anaiacha nyumba yake na kuwaachia watumishi wake kuiangalia, kila mtu na kazi yake, kisha akamwamuru yule bawabu aliye mlangoni akeshe.
35 Kwa hiyo iweni macho! Kwani hamjui ni lini bwana wa nyumba atakaporudi nyumbani, yawezekana ni jioni, usiku wa manane, wakati jogoo atakapowika, au asubuhi.
“Basi kesheni kwa sababu hamjui ni lini mwenye nyumba atakaporudi: iwapo ni jioni, au ni usiku wa manane, au alfajiri awikapo jogoo, au mapambazuko.
36 Kama akija ghafla, asikukute umelala.
Kama akija ghafula, asije akawakuta mmelala.
37 Kile nikisemacho kwako nakisema kwa kila mtu: Kesheni”!
Lile ninalowaambia ninyi, nawaambia watu wote: ‘Kesheni!’”

< Marko 13 >