< Luka 16 >

1 Yesu aliwaambia tena wanafunzi wake, “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyekuwa na meneja, na alitaarifiwa ya kwamba meneja huyu anatapanya mali zake. 2 Hivyo tajiri akamwita, akamwambia, “Ni nini hii ninayo isikia juu yako? Toa hesabu ya umeneja wako, kwa kuwa huwezi kuwa meneja tena.' 3 Yule meneja akasema moyoni mwake, Nifanye nini, maana bwana wangu ananiondolea kazi yangu ya umeneja? Sina nguvu za kulima, na kuomba naona haya. 4 Najua nitakalotenda ili nitakapotolewa katika kazi yangu ya uwakili watu wanikaribishe nyumbani mwao. 5 Hivyo wakili akawaita wadeni wa bwana wake kila mmoja akamwambia wa kwanza, 'unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?' 6 Akasema vipimo mia moja vya mafuta akamwambia 'chukua hati yako keti upesi andika hamsini.' 7 kisha akamwambia mwingine na wewe unadaiwa kiasi gani?' akasema 'vipimo mia moja vya unga vya ngano.' Akamwambia 'twaa hati yako andika themanini.' 8 Yule bwana akamsifu meneja dhalimu kwa vile alivyotenda kwa wereu. Kwakua watoto wa ulimwengu huu ni werevu nyingi na hushughulika kwa ujanja na watu wa upande wao kuliko walivyo watoto wa nuru. (aiōn g165) 9 Nami nawaambia jifanyieni marafiki kwa mali ya udhalimu ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. (aiōnios g166) 10 Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia. na aliye dhalimu katika lililo dogo huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. 11 Kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu ni nani atakayewaamini katika mali ya kweli? 12 Na kama hamkuwa waaminifu katika kutumia mali ya mtu mwingine ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? 13 Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili, kwamaana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamuwezi kumtumikia Mungu na mali.” 14 Basi Mafarisayo, ambao walikuwa wanapenda fedha waliyasikia haya yote na wakamdhihaki. 15 Na akawaambia, “Ninyi ndiyo mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu. 16 Sheria na manabii vilikuwapo mpaka Yohana alivyokuja. Tangu wakati huo, habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujaribu kujiingiza kwa nguvu. 17 Lakini ni rahisi kwa mbingu na nchi vitoweke kuliko hata herufi moja ya sheria ikosekane. 18 Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini, naye amwooaye yeye aliyeachwa na mumewe azini. 19 Palikua na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi na alikua akifurahia kila siku utajiri wake mkubwa. 20 Na maskini mmoja jina lake Lazaro aliwekwa getini pake, na ana vidonda. 21 Naye alikua akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri hata mbwa wakaja wakamlamba vidonda vyake. 22 Ikawa yule maskini alikufa na akachukuliwa na Malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa akazikwa. 23 Na kule kuzimu alipokua katika mateso aliyainua macho yake akamuona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro kifuani mwake. (Hadēs g86) 24 Akalia akasema, 'Baba Ibrahimu, nihurumue umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. 25 Lakini Ibrahimu akasema, 'Mwanangu kumbuka ya kwamba katika maisha yako uliyapokea mambo yako mema, na Lazaro vivyo alipata mabaya. Ila sasa yupo hapa anafarijiwa na wewe unaumizwa. 26 Na zaidi ya hayo, kumewekwa shimo kubwa na refu kati yetu, ili wale wanaotaka kutoka huku kwenda kwenu wasiweze wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.' 27 Yule tajiri akasema, 'Nakuomba Baba Ibrahimu, kwamba umtume nyumbani kwa baba yangu 28 kwa kuwa ninao ndugu watano ili awaonye, kwa hofu kwamba wao pia watkuja mahali hapa pa mateso. ' 29 Lakini Ibrahimu akasema, 'Wanao Musa na manabii. Waache wawasikilize wao. 30 Yule tajiri akasema, 'hapana, Baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu watatubu.' 31 Lakini Ibrahimu akamwambia, 'wasipowasikia Musa na manabii hawatashawishiwa hata mtu akifufuka katika wafu.

< Luka 16 >