< Luka 16 >

1 Yesu aliwaambia tena wanafunzi wake, “Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyekuwa na meneja, na alitaarifiwa ya kwamba meneja huyu anatapanya mali zake.
Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Ilisemekana kwamba huyo msimamizi alikuwa anatumia vibaya mali ya tajiri yake.
2 Hivyo tajiri akamwita, akamwambia, “Ni nini hii ninayo isikia juu yako? Toa hesabu ya umeneja wako, kwa kuwa huwezi kuwa meneja tena.'
Hivyo huyo tajiri akamwita na kumuuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’
3 Yule meneja akasema moyoni mwake, Nifanye nini, maana bwana wangu ananiondolea kazi yangu ya umeneja? Sina nguvu za kulima, na kuomba naona haya.
“Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba.
4 Najua nitakalotenda ili nitakapotolewa katika kazi yangu ya uwakili watu wanikaribishe nyumbani mwao.
Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani kwao.’
5 Hivyo wakili akawaita wadeni wa bwana wake kila mmoja akamwambia wa kwanza, 'unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?'
“Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamuuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’
6 Akasema vipimo mia moja vya mafuta akamwambia 'chukua hati yako keti upesi andika hamsini.'
“Akajibu, ‘Galoni 800za mafuta ya mizeituni.’ “Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike galoni 400.’
7 kisha akamwambia mwingine na wewe unadaiwa kiasi gani?' akasema 'vipimo mia moja vya unga vya ngano.' Akamwambia 'twaa hati yako andika themanini.'
“Kisha akamuuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’ “Akajibu, ‘Vipimo 1,000vya ngano.’ “Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, andika vipimo 800!’
8 Yule bwana akamsifu meneja dhalimu kwa vile alivyotenda kwa wereu. Kwakua watoto wa ulimwengu huu ni werevu nyingi na hushughulika kwa ujanja na watu wa upande wao kuliko walivyo watoto wa nuru. (aiōn g165)
“Yule bwana akamsifu yule msimamizi dhalimu kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru. (aiōn g165)
9 Nami nawaambia jifanyieni marafiki kwa mali ya udhalimu ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. (aiōnios g166)
Nawaambia, tumieni mali ya kidunia kujipatia marafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele. (aiōnios g166)
10 Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia. na aliye dhalimu katika lililo dogo huwa dhalimu katika lililo kubwa pia.
“Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu hata katika mambo makubwa, naye mtu ambaye si mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa.
11 Kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu ni nani atakayewaamini katika mali ya kweli?
Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli?
12 Na kama hamkuwa waaminifu katika kutumia mali ya mtu mwingine ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
13 Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili, kwamaana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamuwezi kumtumikia Mungu na mali.”
“Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali.”
14 Basi Mafarisayo, ambao walikuwa wanapenda fedha waliyasikia haya yote na wakamdhihaki.
Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau.
15 Na akawaambia, “Ninyi ndiyo mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.
Yesu akawaambia, “Ninyi mnajionyesha kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo.
16 Sheria na manabii vilikuwapo mpaka Yohana alivyokuja. Tangu wakati huo, habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujaribu kujiingiza kwa nguvu.
“Sheria na Manabii vilihubiriwa mpaka kuja kwa Yohana Mbatizaji. Tangu wakati huo habari njema za Ufalme wa Mungu zinahubiriwa, na kila mmoja hujiingiza kwa nguvu.
17 Lakini ni rahisi kwa mbingu na nchi vitoweke kuliko hata herufi moja ya sheria ikosekane.
Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Sheria.
18 Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini, naye amwooaye yeye aliyeachwa na mumewe azini.
“Mtu yeyote amwachaye mkewe na kumwoa mwanamke mwingine anazini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa anazini.
19 Palikua na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi na alikua akifurahia kila siku utajiri wake mkubwa.
“Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku.
20 Na maskini mmoja jina lake Lazaro aliwekwa getini pake, na ana vidonda.
Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima.
21 Naye alikua akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri hata mbwa wakaja wakamlamba vidonda vyake.
Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake.
22 Ikawa yule maskini alikufa na akachukuliwa na Malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa akazikwa.
“Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Abrahamu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa.
23 Na kule kuzimu alipokua katika mateso aliyainua macho yake akamuona Ibrahimu kwa mbali na Lazaro kifuani mwake. (Hadēs g86)
Kule kuzimu alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Abrahamu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa karibu yake. (Hadēs g86)
24 Akalia akasema, 'Baba Ibrahimu, nihurumue umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.
Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Abrahamu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’
25 Lakini Ibrahimu akasema, 'Mwanangu kumbuka ya kwamba katika maisha yako uliyapokea mambo yako mema, na Lazaro vivyo alipata mabaya. Ila sasa yupo hapa anafarijiwa na wewe unaumizwa.
“Lakini Abrahamu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu.
26 Na zaidi ya hayo, kumewekwa shimo kubwa na refu kati yetu, ili wale wanaotaka kutoka huku kwenda kwenu wasiweze wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.'
Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’
27 Yule tajiri akasema, 'Nakuomba Baba Ibrahimu, kwamba umtume nyumbani kwa baba yangu
“Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yangu,
28 kwa kuwa ninao ndugu watano ili awaonye, kwa hofu kwamba wao pia watkuja mahali hapa pa mateso. '
maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’
29 Lakini Ibrahimu akasema, 'Wanao Musa na manabii. Waache wawasikilize wao.
“Abrahamu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Mose na Manabii, wawasikilize hao.’
30 Yule tajiri akasema, 'hapana, Baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu watatubu.'
“Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Abrahamu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’
31 Lakini Ibrahimu akamwambia, 'wasipowasikia Musa na manabii hawatashawishiwa hata mtu akifufuka katika wafu.
“Abrahamu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Mose na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’”

< Luka 16 >