< Yoshua 2 >

1 Kisha Yoshua mwana wa Nuni aliwatuma watu wawili kwa siri kama wapelelezi kutoka Shitimu. Akisema, “Nendeni mkaiangalie nchi, hasa Yeriko.” Walienda na wakafika katika nyumba ya kahaba ambaye jina lake ni Rahabu, na wakalala hapo. 2 Mfalme wa Yeriko aliambiwa, “Tazama watu wa Israeli wamekuja kuipeleleza nchi.” 3 Mfalme akatuma neno kwa Rahabu kusema, “Watoe watu waliokuja kwako ambao wameingia nyumbani mwako, kwa kuwa wamekuja kuipeleleza nchi yote.” 4 Lakini mwanamke alikuwa amekwisha kuwachukua wale watu wawili na kuwaficha. Na akasema, “Ndiyo, watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka. 5 Ilipokuwa jioni wakati wa kufungwa kwa lango la mji, waliondoka. Sijui mahali walikoelekea. Mnaweza kuwakamata kama mtawafuata upesi. 6 Lakini yeye aliwapandisha juu darini na kuwaficha kwa mabua ya kitani ambayo alikuwa ameyalaza darini. 7 Hivyo, watu waliwafuatilia njiani iliyoeleka katika vivuko vya Yordani. Na milango ilifungwa mara tu baada ya wale watu waliofuata kutoka nje. 8 Wale wanaume walikuwa hajalala usiku, wakati alipowaendea kule darini. 9 Akawaambia, “Ninajua kwamba Yahweh amewapa ninyi nchi na kwamba hofu juu yenu imetuingia. Watu wote wanaoishi katika nchi watayeyuka mbele yenu. 10 Tumesikia jinsi ambavyo Yahweh alivyokausha maji ya Bahari ya Mianzi kwa ajili yenu wakati mkitoka Misri. Na tumesikia mlichokifanya kwa wafalme wawili wa Waamori walioko upande mwingine wa Yordani - Sihoni na Ogu - ambao mmewaangamiza kabisa. 11 Mara tu tuliposikia, mioyo yetu iliyeyuka na hapakuwa na ujasiri wowote uliosalia kwa mtu yeyote - kwa kuwa Yahweh Mungu wenu, ni Mungu aliye juu mbinguni na chini duniani. 12 Sasa basi, tafadhali mniapie kwa Yahweh kwamba kama nilivyokuwa mwema kweu, nanyi pia mtaitendea mema nyumba ya baba yangu. Nipeni ishara ya uhakika 13 kwamba mtanihifadhi maisha ya baba, mama, kaka, dada zangu na famiie zao, na kwamba mtatuokoa kutoka katika kifo. 14 Wanaume wakamjibu, “maisha yetu kwa ajili ya yenu, hata kifo! Kama hamtasema habari zetu, na Yahweh akisha kutupa nchi hii, tutakuwa wenye huruma na waaminifu kwenu.” 15 hivyo aliwashusha chini kwa kupitia dirishani kwa kutumia kamba. Nyumba ambayo alikuwa anaishi ilijengwa katika ukuta wa mji. 16 Akawaambia, “Nendeni milimani la sivyo watu waliowafuata watawaona. Jificheni huko kwa siku tatu mpaka watu waliowafuata watakaporudi. Kisha nendeni zenu.” 17 Wanaume wakamwambia, “Hatutakuwa tumefungwa na ahadi ulizotufanya tuape mbele zako, kama hautalifanya hili. 18 Tutakapokuja katika nchi, ni lazima uifunge kamba hii nyekundu katika dirisha ulilotushushia chini, na utawakusanya katika nyumba baba yako, mama yako, kaka zako na wote wa nyumba ya baba yako. 19 Na yeyote aendaye mtaani nje ya milango ya nyumba yako, damu yao itakuwa juu ya vichwa vyao na hatutakuwa na hatia yoyote. Lakini kama mkono utanyoshwa juu ya mtu yeyote aliye pamoja nawe katika nyumba, damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu. 20 Na ikiwa utaongea juu ya suala letu, tutakuwa huru dhidi ya kiapo ulichotuapisha. 21 Rahabu akawajibu, “Yote mliyosema nayatimie.” Akawatoa mbali na wakaondoka. Kisha akaifunga kamba nyekundu katika dirisha. 22 Wakaondoka na kwenda juu milimani na walikaa huko kwa siku tatu hadi pale wale waliowafuatilia waliporudi. Wale waliowafuata walitafuta njiani pote bila kuwaona. 23 Wale watu wawili walirudi na kuvuka mto na wakafika kwa Yoshua mwana wa Nuni, na walimwambia kila kitu kilichotokea kwao. 24 Nao wakasema kwa Joshua, “kwa kweli Yahweh ametupa nchi hii. Wenyeji wote wa nchi wanayeyuka kwasababu yetu.

< Yoshua 2 >