< Ayubu 7 >

1 Je mtu hana kazi ngumu juu ya nchi? Je siku zake si kama siku za mwajiriwa? 2 Kama mtumwa atamaniye sana kivuli cha jioni, kama mwajiriwa atafutaye ujira wake - 3 hivyo nami nimeumbwa kuvumilia miezi ya taabu; Nami nimepewa taabu - zimeujaza usiku. 4 Hapo nilalapo chini, najiuliza mwenyewe, 'Lini nitatoka kitandani na lini usiku utatoweka?' Nimejawa na kujitupa huku na huko hadi mwanzo wa siku. 5 Mwili wangu umevikwa minyoo na madonda yenye vumbi; maumivu katika ngozi yangu yamekuwa magumu na kisha hutoweka na huendelea tena. 6 Siku zangu zinakimbia kuliko chombo cha kufumia; zinapita bila tumaini. 7 Mungu, anakumbuka kwamba maisha yangu ni pumzi tu; jicho langu halitaona mema tena. 8 Jicho lake Mungu, huyo anionaye mimi, halitaniangalia tena; Macho ya Mungu yatanitazama, lakini sitakuwako. 9 kama vile wingu liishavyo na kutoweka, hivyo wale waendao sheoli hawatarudi tena kabisa. (Sheol h7585) 10 Yeye hatarudi tena nyumbani kwake, wala mahali pake hapatamtambua tena. 11 Kwa sababu hiyo sitakizuia kinywa changu; Nitasema juu ya maumivu makubwa ya roho yangu; Nitanung'unika juu ya uchungu wa nafsi yangu. 12 Je mimi ni bahari au kiumbe cha kutisha baharini hata ukaweka mlinzi juu yangu? 13 Hapo nisemapo, 'kitanda changu kitanifariji, na malazi yangu yatatuliza manung'uniko yangu,' 14 halafu unitishapo kwa ndoto na kunitisha kwa maono, 15 ili nichague kunyongwa na kufa kuliko kulinda mifupa yangu hii. 16 Ninayachukia kabisa maisha yangu; sitamani siku zote kuwa hai; usinisumbue maana siku zangu hazifai. 17 Je mtu ni nini hata ukatia bidii kwake, na ukaweka akili yako kwake, 18 na kumwangalia kila asubuhi, na kumjaribu kila mara? 19 Je itachukuwa muda gani kabla hujaacha kuniangalia, wala kunisumbua muda wa kutosha kwaajili ya kumeza mate yangu? 20 Hata kama nimefanya dhambi, itakusaidia nini, wewe ulindaye wanadamu? Kwa nini umenifanya shabaha yako, kiasi kwamba nimekuwa mzigo kwako? 21 Kwa nini hunisamehi makosa yangu na kuniondolea uovu wangu? kwa kuwa sasa nitalala mavumbini; na wewe utanitafuta kwa bidii, lakini sitakuwako.”

< Ayubu 7 >