< Ayubu 40 >

1 Yahweh aliendelea kuongea na Ayubu na kusema, 2 “Je mtu yeyote anayetaka kukosoa na ajaribu kumsahihisha Mwenye enzi? Na yeye anayehojiana na Mungu, na ajibu yeye.” 3 Ndipo Ayubu akamjibu Yahweh na kusema, “ 4 Tazama, mimi si mtu muhimu; je nawezaje kukujibu? Ninauweka mkono wangu juu ya mdomo wangu. 5 Ninazungumza mara moja, na sitakujibu; hakika, mara mbili, lakini sitaendelea zaidi.” 6 Kisha Yahweh akamjibu Ayubu kutoka katika dhoruba kali na kusema, 7 “Jifunge sasa mkanda kiunoni mwako kama mwanaume, kwa kuwa nitakuuliza maswali, nawe lazima unijibu. 8 Je waweza kusema kwa hakika kwamba mimi si mwenye haki? Je utanihukumu mimi ili useme wewe ni mwenye haki? 9 Je una mkono kama wa Mungu? Je waweza kutoa kishindo kwa sauti kama yeye? 10 Jivike sasa katika utukufu na katika utu; jivalie mwenyewe heshima na enzi. 11 Sambaza ziada ya hasira yako; mtazame kila mmoja mwenye kiburi na umshushe chini. 12 Mwangalie kila mmoja mwenye kiburi na umweke chini; wakanyage chini watu waovu mahali wanaposimama. 13 Wazike ardhini pamoja; zifunge nyuso zao katika sehemu zilizositirika. 14 Ndipo pia nitakapokubali ya kwamba mkono wako wa kulia waweza kukuokoa. 15 Mwangalie sasa kiboko, ambaye niliwafanya kama nilivyokufanya wewe; anakula nyasi kama ng'ombe. 16 Ona sasa, nguvu zake ziko katika viuno vyake; nguvu zake zi katika mishipa ya tumbo lake. 17 Yeye huuondoa mkia wake kama mti wa mwerezi; mishipa ya paja lake imeunganishwa pamoja. 18 Mifupa yake ni kama ya mirija ya shaba; na miguu yake ni kama kipande cha chuma. 19 Yeye ni mkuu wa viumbe vya Mungu. Ni Mungu pekee, ambaye alimwumba, anaweza kumshinda. 20 Kwa kuwa milima humpatia chakula; hayawani wa mashambani hucheza karibu. 21 Hujilaza chini ya mimiea ya kivuli katika makao ya mianzi, na katika bwawa la matope. 22 Miti yenye vivuli humfunika katika vivuli vyake; mierebi ya kijito inamzunguka pande zote. 23 Tazama, kama mto utazigharikisha kingo zake, hatikisiki; yeye anajiamini, hata kama Mto wa Yordani unajaa hadi katika pua yake. 24 Je mtu yeyote aweza kumnasa kwa ndoano, au kuichoma pua yake kwa mtego?

< Ayubu 40 >