< Ayubu 36 >

1 Elihu aliendelea na kusema, 2 “Niruhusu niseme kidogo zaidi, nami nitakuonesha baadhi ya mambo kwasababu nina maneno machache ya kusema kwa ajili ya Mungu. 3 Nitapata maarifa yangu kutoka mbali; nitatambua kwamba haki ni ya Muumba wangu. 4 Kwa kweli, maneno yangu hayatakuwa ya uongo; mtu fulani aliyekomaa katika maarifa yu pamoja nawe. 5 Angalia, Mungu ni mwenye nguvu, na hamdharau mtu yeyote; yeye ni mwenye nguvu katika uweza wa ufahamu. 6 Yeye huwa hayahifadhi maisha ya watu waovu bali badala yake hufanya yaliyo ya haki kwa wale wanaoteseka. 7 Haondoi macho yake kwa wenye haki bali badala yake huwaweka juu ya viti vya enzi kama wafalme milele, nao wameinuliwa juu. 8 Ikiwa wamefungwa minyororo na kunaswa katika kamba za mateso, 9 kisha huwafunulia kile walichokifanya, na maovu yao na kiburi chao. 10 Hufungua pia masikio yao kwa ajili ya agizo lake, na huwaamuru wageuke kutoka katika uovu. 11 Ikiwa watamsikiliza na kumwabudu yeye, wataishi katika mafanikio katika siku zao, na miaka yao katika hali ya kuridhika. 12 Hata hivyo, kama hawatasikiliza, wataangamia kwa upanga; watakufa kwasababu hawana maarifa. 13 Na wale wasiomjua Mungu hutunza hasiria zao katika mioyo; hawaombi msaada hata wakati ambapo Mungu huwafunga. 14 Hawa hufa katika ujana wao; na maisha yao hukoma kati ya makahaba. 15 Mungu huwainua watu walioonewa kwa njia ya mateso yao; hufungua masikio yao kwa njia ya uonevu wao. 16 Kwa hakika, yeye angependa kuwatoa ninyi katika mateso na kuwaweka katika sehemu pana ambapo hakuna masumbufu na mahali ambapo meza yenu ingewekwa ikiwa na chakula kilichojaa mafuta. 17 Lakini wewe umejaa hukumu juu ya watu waovu; hukumu na haki umeziachilia. 18 Usiuache utajiri ukuvute katika udanganyifu; na sehemu kubwa ya rushwa isikugeuze upande kutoka katika haki. 19 Je utajiri wako waweza kukunufaisha, ili kwamba usiwe katika taabu, au nguvu zako zote za uwezo zaweza kukusaidia? 20 Usiutamani usiku ili utende dhambi dhidi ya wengine wakati ambapo mataifa hukatiliwa mbali katika nafasi zao. 21 Uwe mwangalifu ili kwamba usigeukie dhambi kwasababu unajaribiwa kwa mateso ili kwamba ukae mbali na dhambi. 22 Angalia, Mungu ameinuliwa katika nguvu zake; ni nani aliye mwalimu kama yeye? 23 Ni nani alishamwalekeza njia yake? Nani anayeweza kumwambia, 'Wewe umetenda mambo yasiyo ya haki?' 24 Kumbuka kuyasifu matendo yake, ambayo watu wameyaimba. 25 Watu wote wameshayatazama hayo matendo, lakini wanayaona tu matendo hayo kwa mbali sana. 26 Tazama, Mungu ni mkuu, lakini sisi hatumfahamu yeye vizuri; hesabu ya miaka yake haihesabiki. 27 Kwa kuwa yeye huvuta matone ya maji ili kuyachuja kama mvua katka mvuke wake, 28 ambayo mawingu yake huyamwaga chini na kuyandondosha kwa wingi kwa mwanadamu. 29 Hakika, kuna hata mmoja awezaye kuelewa kwa undani kusambaa kwa mawingu na radi kutoka katika nyumba yake? 30 Angalia, hueneza mwanga wake kumzunguka na kufunika mizizi ya bahari. 31 Kwa namna hii huyahukumu mataifa na kuwapa chakula kwa wingi. 32 Yeye huuijaza mikono yake kwa mwanga mpaka pale anapouamuru kupiga shabaha yake. 33 Na muungurumo wake huonya kwa dhoruba, wanyama wanaweza kusikia kuja kwake.

< Ayubu 36 >