< Ayubu 30 >

1 Sasa vijana wananidhihaki - vijana ambao baba zao wasingeweza hata kuwahudumia mbwa wa kundi langu. 2 Kwa kweli, nguvu za mikono ya baba zao, zingenisaidia nini - watu ambao hawakuwa na nguvu wakati wa kukua kwao? 3 Walidhoofishwa na umasikini na njaa; walisaga nchi kavu mafichoni. 4 Walichuma mche chumvi na majani ya vichaka; mizizi ya mti wa ufagio ilikuwa ndiyo chakula chao. 5 Waliondolewa miongoni mwa watu waliopiga kelele nyuma yao kama ambavyo mtu angempigia kelele mwizi. 6 Hivyo walipaswa kuishi katika mabonde ya mto, katika mashimo ya ardhi na miamba. 7 Walilia kwa uchungu porini kama punda; chini ya vichaka walikutana. 8 Walikuwa uzao wa wapumbavu, hakika, wa watu wasiofaa; waliondolewa duniani kama waarifu. 9 Lakini sasa, nimekua sababu ya wimbo wa dhihaka kwa wana wao; hakika, nimekuwa mzaa kwao. 10 Wananichukia na kusimama mbali nami; hawaachi kunitemea usoni. 11 Kwa maana Mungu ameondoa kamba katika upinde wangu na amenipiga, na hivyo watu hawa wanashindwa kujizuia mbele yangu. 12 Kundi la vijana wabaya wanashambulia nguvu zangu; wananiondolea mbali na kukusanya kinyume changu rundo la kuhusuru. 13 Wanaharibu maisha yangu; wanapeleka mbele maangamizi yangu, watu wasio na wakuwazuia. 14 Wanakuja kinyume changu kama jeshi katika tundu pana katika ukuta wa mji; katikati ya maangamizi wanajizungusha juu yangu. 15 Hofu zimeniandama; heshima yangu imeondolewa mbali nami kama kwa upepo; mafanikio yangu yameondolewa kama wingu. 16 Sasa uhai wangu umeondolewa ndani yangu; siku nyingi za maumivu zimenipita. 17 Mifupa inauma ndani yangu wakati wa usiku; maumivu yanayonisaga hayaishi. 18 Nguvu kuu ya Mungu imeshika mavazi yangu; yananizunguka kama kala ya vazi langu. 19 Amenitupa matopeni; nimekuwa kama vumbi na majivu. 20 Nakulilia wewe, Mungu, lakini haunijibu; ninasimama, nawe unaniangalia tu. 21 Umegeuka na kuwa mkali kwangu; kwa nguvu za mkono wako umenitesa. 22 Unaniinua katika upepo na kuufanya unikokote; unanirusha huku na kule katika dhoruba. 23 Kwa maana najua ya kwamba utanipeleka mautini, nyumba ya hatima kwa viumbe vyote. 24 Lakini, je hakuna ainuaye mkono wake kuomba msaada aangukapo? Je hakuna aombaye msaada akiwa tabuni? 25 Je sikulia kwa ajili yake aliyekuwa tabuni? Je sijahuzunika kwa ajili ya mwitaji? 26 Nilipotazamia mema, ndipo yalipokuja mabaya; niliposubiri nuru, giza lilikuja badala yake. 27 Moyo wangu umetaabika na hautulii; siku za mateso zimenipata. 28 Nimekuwa na ngozi nyeusi lakini si kwa sababu ya jua; nasimama katika kusanyiko na kulilia msaada. 29 Nimekuwa ndugu kwa mbwea, mshirika wa mbuni. 30 Ngozi yangu imekuwa nyeusi na inapukutika; mifupa yangu imeunguzwa na joto. 31 Kwa hiyo kinubi changu kimefunguliwa kwa nyimbo za maombolezo, zomari yangu kwa kuimba kwao waombolezao.

< Ayubu 30 >