< Ayubu 10 >

1 Nimechoka na maisha yangu; Nitanena wazi manung'uniko yangu; nitasema kwa uchungu wa roho yangu. 2 Nitamwambia Mungu, 'Usinihukumie makosa; nionyeshe sababu za wewe kunilaumu mimi. Je 3 ni vizuri kwako wewe kunionea mimi, kudharau kazi ya mikono yako wakati unafurahia juu ya mipango ya waovu? 4 Je wewe una macho ya kimwili? Je wewe unaona kama mtu aonavyo? 5 Je siku zako ni kama siku za wanadamu au miaka yako ni kama miaka ya watu, 6 hata ukauliza habari za uovu wangu na kuitafuta dhambi yangu, 7 ingawa wewe wafahamu mimi sina kosa na hapana mwingine awezaye kuniokoa mimi na mkono wako? 8 Mikono yako imeniumba na kunifinyanga kwa wakati mmoja nawe kunizunguka, hata hivyo unaniangamiza. 9 Kumbuka, nakuomba, ulivyonifinyanga kama vile udongo; je utanirudisha mavumbini tena? 10 Je wewe hukunimimina kama maziwa na kunigandisha mfano wa jibini? 11 Umenivika ngozi na nyama na kuniunganisha pamoja kwa mifupa na misuli. 12 Wewe umenizawadia mimi uhai na ahadi ya upendeleo na usaidizi wako umeilinda roho yangu. 13 Hata hivyo mambo haya uliyaficha moyoni mwako - nafahamu kwamba hivi ndivyo ufikirivyo: 14 kuwa kama nimefanya dhambi, wewe utaizingatia; hutaniachilia na uovu wangu. 15 Kama mimi ni muovu, ole wangu; hata kama ni mwenye haki, sitaweza kuinua kichwa changu, kwa kuwa nimejaa aibu na kuyaangalia mateso yangu. 16 Kama kichwa changu kikijiinua chenyewe, waniwinda kama simba; tena wajionyesha mwenyewe kuwa ni mwenye nguvu kwangu. 17 Wewe unaleta mashahidi wapya dhidi yangu na kuzidisha hasira zako dhidi yangu; wanishambulia na majeshi mapya. 18 Kwa nini, basi, ulinitoa tumboni? Natamani ningekata roho na ili jicho lolote lisinione. 19 Ningelikuwa kama asiyekuwepo; ningelichukuliwa kutoka tumboni mpaka kaburini. 20 Je si siku zangu pekee ni chache? Acha basi, usinisumbue, ili kwamba nipate kupumzika kidogo 21 kabla sijaenda huko ambako sitarudi, kwenye nchi ya giza na kivuli cha mauti, 22 ni nchi ya giza kama usiku wa manane, nchi ya kivuli cha mauti, isiyokuwa na mpangilio, ambayo nuru yake ni kama usiku wa manane.'”

< Ayubu 10 >