< Yeremia 50 >

1 Hili ni neno alilolisema Yahwe juu ya Babeli, nchi ya Wakalidayo, kwa mkono wa Yeremia nabii, 2 “Wajulishe mataifa ili wasikie. Toa ishara ili wasikie. Usiiache. Sema, 'Babeli imetwaliwa. Beli ameaibika. Merodaki amefadhaika. Sanamu zake zimeaibishwa; vinyago vyake vimefadhaika 3 Taifa kutoka kaskazini litainuka kinyume chake, ili kuifanya nchi yake ukiwa. Hakuna hata mmoja, awe mtu au mnyama, atakayeishi ndani yake. Wataondoka. 4 Katika siku hizo na wakati huo - hili ni tamko ya Yahwe - watu wa Israeli na watu wa Yuda watakusanyika ili kwenda kwa kulia na kumtafuta Yahwe Mungu wao. 5 Watauliza njia ya kwenda Sayuni nao watakwenda huko, wakisema, tutakwenda wenyewe ili kuungana na Yahwe katika agano la milele lisilosahaulikal 6 Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea. Wachungaji wao wamewapoteza milimani; wamewageuza kutoka mlima hata mlima. Walikwenda, wakasahau mahali walipokuwa wanaishi. 7 Kila awaendeaye anawararua. Washitaki wao walisema, 'Hatuna hatia, kwa sababu walimtenda dhambi Yahwe, nyumbani kwao halisi - Yahwe, tumaini la mababu zao.' 8 Tokeni kati ya Babeli; tokeni katika nchi ya Wakalidayo; iweni kama wafanyavyo mabeberu mbele ya kundi lote. 9 Maana tazama, ninaelekea kupeleka na kuinua kinyume cha Babeli kundi la mataifa makubwa kutoka kaskazini. Yatajipanga yenyewe kinyume chake. Kutoka hapo Babeli utatekwa. Mishale yao ni kama shujaa mzoefu asiyerudi mikono tupu. 10 Ukaldayo itakuwa mateka. Wate waitekao wataridhika - asema Yahwe. 11 Mnafurahi, mnasherehekea kuteka urithi wangu; mnarukaruka kama ndama anayekanyaga katika malisho yake; mnalia kama farasi mwenye nguvu. 12 Hivyo mama yenu ataaibika sana; aliyewazaa atafadhaika. Tazama, atakuwa wa mwisho katika mataifa, nyika, nchi kame, na jangwa. 13 Kwa sababu ya hasira ya Yahwe, Babeli haitakaliwa, lakini itakuwa ukiwa mtupu. Kila apitaye kando ataogopa kwa sababu ya Babeli na atatoa sauti kwa sababu ya majeraha yake. 14 Jipangeni wenyewe kumzunguka Babeli kinyume chake. Kila apindaye upinde na ampige. Msizuie mshale wenu wowote, maana amemtenda dhambi Yahwe. 15 Pigeni kelele za ushindi kinyume chake ninyi nyote mmzungukao. Amesalimu mamlaka yake; minara yake imeanguka. Kuta zake zimebomolewa, maana hiki ni kisasi cha Yahwe. Jilipizeni kisasi juu yake! Mtendeeni kama alivyoyatenda mataifa mengine. 16 Waaribuni wote mkulima apandaye mbegu naye atumiaye mundu wakati wa mavuno katika Babeli. Haya kila mtu na arudi kwa watu wake kutoka upanga wa mtesaji; na wakimbilie katika nchi yao wenyewe. 17 Israeli ni kondoo aliyetawanywa na kupelekwa na simba mbali. Kwanza mfalme wa Ashuru alimrarua; kisha baadaye, Nebukadneza mfalme wa Babeli akavunja mifupa yake. 18 Kwa hiyo Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Tazama, nitamwadhibu mfalme wa Babeli na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru. 19 Nitamrudisha Israeli katika nchi yake; atajilisha katika Karmeli na Bashani. Kisha atajishibisha katika nchi ya kilima ya Efraimu na Gileadi. 20 Siku hizo na wakati huo, asema Yahwe, uovu utatafutwa katika Israeli, lakini hautaonekana. Nitauliza kuhusu dhambi za Yuda, lakini hazitaonekana, maana nitawasamehe mabaki niliowaacha.” 21 Inuka dhidi ya nchi ya Merathaimu, kinyume chake nao waishio Pekodi. Wapigeni kwa makali ya upanga na mwatenge kwa ajili ya maangamizo - asema Yahwe - fanyeni kila ninachowaamru. 22 Sauti ya vita na maangamizi ya kustaajabisha yamo katika nchi. 23 Jinsi gani nyundo ya mataifa yote imekatiliwa mbali na kuharibiwa. Jinsi Babeli amekuwa kitu cha kushangaza kati ya mataifa. 24 Nimetega mtego dhidi yako. Umenaswa, Babeli, nawe haukutambua! Ulionekana na kukamatwa, tangu uliponidhihaki, Yahwe. 25 Yahwe amefungua ghala lake la silaha na anachukua silaha kwa ajili ya kutekekeleza hasira yake. Kuna kazi kwa ajili ya Yahwe wa majeshi katika nchi ya Wakaldayo. 26 Mshambulie kutokea mbali. Fungua maghala yake ya chakula na kumrundika kama marundo ya nafaka. Mtenge mbali na maangamizi. Usimbakizie masalia. 27 Ua madume wake wote wa ng'ombe. Washushe sehemu ya machinjio. Ole wao, maana siku yao imefika - wakati wa kuadhibiwa kwao. 28 Kuna sauti ya wale wanaokimbia, walionusurika, katika nchi ya Babeli. Hawa watatoa taarifa ya kisasi cha Yahwe Mungu wetu kwa Sayuni, kisasi kwa hekalu lake.” 29 Ita wapiga pinde dhidi ya Babeli - wale wote wapindao pinde zao. Piga kambi kinyume chake, na msimwache yeyote kutoroka. Mlipeni kwa kile alichofanya. Mfanyieni kwa kipimo alichotumia. Maana amemdharau Yahwe, Mtakatifu wa Israeli. 30 Hivyo vijana wake wataanguka katika viwanja vya mji, na wapiganaji wake wote wataangamizwa siku hiyo - hili ni tamko la Yahwe.” 31 Tazama, mimi ni kunyume chako, mwenye majivuno - hili ni tamko la Bwana Yahwe wa majeshi - maana siku yako imefika, mwenye kiburi, wakati nitakapokuadhibu. 32 Hivyo wenye kiburi watajikwaa na kuanguka. Hakuna atakaye wainua. Nitawasha moto katika miji yao; utateketeza kila kitu kati yake. 33 Yahwe wa majeshi asema hivi: watu wa Israeli wamenyanyaswa, pamoja na watu wa Yuda. Wate waliowateka bado wanawashikilia; wanakataa kuwaacha waondoke. 34 Yeye awaokoaye ni mwenye nguvu. Yahwe wa majeshi ni jina lake. Kwa hakika atalitetea shitaka lao, ili kuleta pumziko katika nchi, na kuwapiga wakaao Babeli. 35 Upanga u juu ya Wakalidayo - asema Yahwe - na juu ya wakaao Babeli, viongozi wake, na wenye hekima wake. 36 Upanga unakuja juu ya waganga, ili wajione kuwa wajinga. Upanga utakuwa juu ya askari wake, hivyo watajaa hofu. 37 Upanga utakuwa juu ya farasi wake, vibandawazi vyao na na watu wote waliomo Babeli, hivyo watakuwa kama wanawake. Upanga utakuwa juu ya ghala zake, nazo zitatekwa. 38 Ukame unakuja juu ya maji yake, hivyo yatakauka. Maana ni nchi ya miungu wasiofaa, na wanafanya kama watu waliofanywa punguani kwa miungu yao isiyosaidia. 39 Hivyo wanyama wa jangwani wakaishi na mbwea wataishi huko, na watoto wa mbuni wataishi ndani yake. Kwa muda wote, hatakaliwa tena. Kutoka kizazi hata kizazi, hatakaliwa tena na watu. 40 Kama vile Mungu alivyoziangamiza Sodoma na Gomora na majirani zake - asema Yahwe - hakuna atakayeishi huko; hakuna mtu atakayekaa ndani yake.” 41 “Tazama, watu wanakuja kutoka kaskazini, maana taifa kubwa na wafalme wengi wamemtikisa kutokea mbali. 42 Watachukua pinde na mishale. Ni wakatili na hawana huruma. Sauti yao ni kama mngurumo wa bahari, na wamepanda farasi katika mpangilio kama watu wapiganao, dhidi yako, bindi Babeli. 43 Mfalme wa Babeli amesikia habari yao na mikono yake imelegea kwa huzuni. Mashaka yamemshika kama mwanamke katika utungu. 44 Tazama! Anakwenda juu kama simba atokaye katika miinuko ya Yordani kuelekea katika eneo la malisho ya uvumilivu. Maana kwa haraka nitawafanya wakimbie kutoka humo, nami nitamweka mtu aliyechaguliwa kwa uangalizi wake. Maana ni nani aliye kama mimi, na ni nani atakayeniagiza? Mchungaji gani awezaye kunizuia? 45 Sikilizeni mipango ambayo Yahwe ameamua juu ya Babeli, mipango aliyonayo dhidi ya nchi ya Wakaldayo. Kwa hakika wataondolewa, hata kundi dogo zaidi. Eneo lao la malisho litageuzwa kuwa sehemu zenye magofu. 46 Kwa sauti ya kuangushwa kwa Babeli nchi inatikisika, na sauti ya mateso yao inasikiwa kati ya mataifa.”

< Yeremia 50 >