< Yeremia 49 >

1 Juu ya watu wa Amoni, Yahwe asema hivi, “Je Israeli hana watoto? Je hakuna mtu wa kurithi chochote katika Israeli? Kwa nini Moleki aikalie Gadi, na watu wake kukaa katika miji yake? 2 Hivyo angalia, siku zinakuja - asema Yahwe - nitakapo sikizisha ishara ya vita juu ya Raba miongoni mwa watu wa Amoni, hivyo itakuwa rundo lililoachwa na binti zake watawasha moto. Maana Israeli atawamiliki wanaommiliki,” asema Yahwe. 3 Piga kelele kwa maombolezo, Heshboni, maana Ai utaangamizwa! Piga kelele, Binti za Raba! Vaeni nguo za magunia. Ombolezeni na kukimbia kwa kuchanganyikiwa, maana Moleki anakwenda matekani, pamoja na makuhani na viongozi wake. 4 Kwa nini mnajivunia nguvu zenu? Nguvu zenu zitakwisha, binti wasioamini, ninyi mnaotumaini utajiri wenu. Mwasema, “Nani atakayekuja kinyume changu?' 5 Tazama, nitaleta kitisho juu yenu - hili ni tamko la Yahwe, Bwana wa majeshi - kitisho hiki kitatoka kwao wote wanaowazunguka. Kila mmoja wenu atatawanyika mbele yake. Hakutakuwa na wa kuwakusanya wanaotawanyika. 6 Lakini baada ya haya nitarejesha mema ya watu wa Amoni - hili ni tamko la Yahwe.” 7 Juu ya Edomu, Yahwe wa majeshi asema hivi, Je hakuna tena hekima katika Temani? Je ushauri mwema umepotea kutoka kwa wenye ufahamu? Je hekima yao imeharibika? 8 Kimbieni! Rudini nyuma! Bakini katika mashimo katika ardhi, wenyeji wa Dedani. Maana naleta maafa ya Esau juu yake wakati ninaomwadhibu. 9 Ikiwa wavunaji wa zabibu walikuja kwako, je wasinge acha kidogo? Ikiwa wezi walikuja usiku, je wasingeiba kiasi walichotaka? 10 Lakini nimempiga Esau kwa ukiwa. Nimefunua maficho yao. Hivyo hataweza kujificha mwenyewe. Watoto wake, ndugu zake, na jirani zake wameharibiwa, wamepotea. 11 Acha nyuma yatima wako. Nitachukua uhai wao, na wajane wako wanaweza kuniamini.” 12 Maana Yahwe asema hivi, “Tazama, wasiostahili ni lazima wanywe sehemu ya kikombe. Je mnadhani mtaachwa bila kuhadhibiwa? Hapana, maana hakika mtakunywa. 13 Maana nimekwisha apa kwangu mimi mwenyewe - asema Yahwe - Hiyo Bozra itakuwa hofu, aibu, magofu, na kitu cha laana. Miji yake yote itakuwa magofu daima. 14 Nimesikia habari kutoka kwa Yahwe, na mjumbe ametumwa katika mataifa, 'Kusanyikeni na kumpiga. Jiandaeni kwa vita.' 15 “Maana tazama, nimekufanya kuwa mdogo kulinganisha na mataifa mengine, yenye kudharauliwa na watu. 16 Na kwa hofu yenu, kiburi cha moyo wako kimekudanganya, wakaaji wa maeneo ya mwinuko, ninyi mliomiliki vilele vya vilima ili mfanye viota vyenu kama tai. Nitawashusha kutoka huko - asema Yahwe. 17 Edomu atakuwa kitisho kwa kila aipitaye. Kila mtu atatetemeka na kutoa sauti kwa sababu ya maafa yake. 18 Kama maangamizi ya Sodoma na Gomora na jirani zake,” asema Yahwe, “hakuna atakayeishi pale; hakuna mtu atakayekaa huko. 19 Tazama, nitapanda kama simba kutoka katika misitu ya Yordani hata eneo la malisho mabichi. Maana nitaharakisha kumfanya Edomu kumkimbia, nami nitamweka mwingine atakayekuwa amechaguliwa kwa usimamizi huo. Maana ni nani aliyekama mimi, ni nani atakayeniagiza kuja? Mchungaji gani awezaye kunizuia? 20 Hivyo sikiliza mipango ambayo Yahwe ameamua dhidi ya Edom, mipango aliyoifanya kinyume cha wakaao Temani. Bila shaka wataondolewa, hata kundi dogo kuliko yote. Nchi yao yenye malisho yao mabichi itageuzwa kuwa sehemu zenye magofu. 21 Kwa kishindo cha kuanguka kwao nchi hutikisika. Sauti ya milio ya kukata tamaa inasikika katika Bahari ya Shamu. 22 Tazama, mtu fulani atapiga kama tai, na kushuka chini kwa kasi na kueneza mabawa yake juu ya Bozra. Kisha katika siku hiyo, mioyo ya askari wa Edomu itakuwa kama moyo wa mwanamke katika kuzaa.” 23 Juu ya Dameski: “Hamathi na Arpadi zitaaibika, maana wamesikia habari ya madhara. Wanayeyuka! Wamesumbuka kama bahari, isiyotulia. 24 Dameski umekuwa dhaifu sana. Unageuka kukimbia; hofu imeushika, Maangaiko na maumivu yameupata, kama uchungu wa mwanamke ajifunguaye. 25 Watu wake wanasema, “Umekuwaje mji maarufu, mji ambao nimeufurahia, kabla haujaachwa? 26 Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika mitaa yake na askari wake wote watateketea siku hiyo - hili ni tamko la Yahwe wa majeshi.” 27 “Maana nitawasha moto katika kuta za Dameski, nami nitazivunja ngome za Beni Hadadi.” 28 Juu ya Kedari na falme za Hazori, Yahwe amwambia hivi Nebukadneza (Basi Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuwa akienda kuyashambulia maeneo haya): “Inuka na uipige Kedari na kuwaharibu wale watu wa mashariki. 29 Jeshi lake litachukua hema zao na makundi yao, nguzo za hema yao, na vitu vyao vyote. Watachukua ngamia wao kutoka kwa watu wa Kedari na kuwambia, 'Hofu ipo pande zote!” 30 Kimbia, Tangatanga mbali! Kaa katika maandaki ardhini, mkaao Hazori - asema Yahwe - maana Nebukadneza mfalme wa Babeli amepanga mpango kinyume chenu. Kimbieni! Geukeni! 31 Simama! lishambulie taifa lililokatika amani, waishio salama,” asema Yahwe. Hawana malango wala nguzo ndani yao, na watu wake wanakaa wenyewe. 32 Maana farasi wao watakuwa mateka, na wingi wa mali zao utakuwa mateka wa vita. Kisha nitawatawanya katika kila upepo wanaonyoa pembe za nywele zao, nami nitaleta madhara juu yao kutoka kila upande - hili ni tamko ya Yahwe. 33 Hazori utakuwa makao ya mbwea, nchi isiyofaa daima. Hakuna atakayeishi huko; hakuna mwanadamu atakayekaa huko.” 34 Hili ni neno la Yahwe lililomwijia Yeremia nabii kuhusu Elamu. Ilikuwa wakati wa mwanzo wa kutawala kwake Sedekia mfalme wa Yuda, naye akasema, 35 “Yahwe wa majeshi asema hivi: Tazama, ninakaribia kumvunja mpiga upinde wa Elamu, sehemu kuu ya nguvu zao. 36 Maana nitaleta pepo nne kutoka katika pande nne za mbingu, nami nitawatawanya watu wa Elamu katika pepo hizo zote. Hakuta kuwa na taifa ambalo kwalo waliotawanywa kutoka Elamu hawatakwenda. 37 Hivyo nitawavunjavunja Elamu mbele ya adui zao na mbele ya watafutao uhai wao. Maana nitaleta maangamizo dhidi yao, hasira ya gadhabu yangu - hili ni tamko la Yahwe - nami nitapeleka upanga nyuma yao hata nitakapowafuta wote. 38 Kisha nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu na kumwangamiza mfalme na viongozi wao kutoka huko - asema Yahwe - 39 na itakuwa siku zijazo kwamba nitarejesha mema ya Elamu - asema Yahwe.”

< Yeremia 49 >