< Mwanzo 50 >

1 Yusufu akahuzunika sana hata akauangukia uso wa baba yake, akamlilia, na kumbusu. 2 Yusufu akawaagiza watumishi wake matabibu kumtia dawa babaye. Hivyo matabibu wakampaka dawa Israeli. 3 Wakatimiza siku arobain, kwani huo ndio uliokuwa muda kamili wa kutia dawa. Wamisri wakamlilia kwa siku sabini 4 Siku za maombolezo zilipotimia, Yusufu akaongea na watumishi wa baraza la kifalme wa Farao kusema, “Ikiwa nimepata kibali machoni penu, tafadharini ongeeni na Farao, kusema, 5 'Baba yangu aliniapisha, kusema, “Tazama, ninakaribia kufa. Unizike katika kaburi nililolichimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani. Ndipo utakaponizika.” Basi sasa niruhusu niende nimzike baba yangu, na kisha nitarudi.” 6 Farao akajibu, “Nenda na umzika baba yako, kama alivyokuwapisha.” 7 Yusufu akaenda kumzika baba yake. Maofisa wa Farao wote wakaenda pamoja naye - washauri wa nyumba yake, maofisa waandamizi wote wa nchi ya Misri, 8 pamoja na nyumba yote ya Yusufu na ndugu zake, na nyumba yote ya baba yake. Lakini watoto wao, kondoo wao na makundi ya mbuzi wao yaliachwa katika nchi ya Gosheni. 9 Vibandawazi na wapanda farasi pia walikwenda pamoja naye. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu. 10 Hata walipokuja katika sakafu ya kupuria ya Atadi upande mwingine wa Yordani, wakaomboleza kwa majonzi ya huzuni kubwa. Yusufu akafanya maombolezo ya siku saba kwa ajili ya babaye pale. 11 Wenyeji wa nchi, Wakanaani, walipoona maombolezo katika sakafu ya Atadi, wakasema, “Hili ni tukio la kuhuzunisha sana kwa Wamisri.” Ndiyo maana eneo hilo likaitwa Abeli Mizraimu, lililoko mbele ya Yordani. 12 Hivyo wanawe wakamfanyia Yakobo kama alivyokuwa amewaagiza. 13 Wana wake wakampeleka katika nchi ya Kanaani na wakamzika katika pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre. Ibrahimi alikuwa amelinunua pango pamoja na shamba kwa ajili ya eneo la kuzikia. Alikuwa amelinunua kutoka kwa Efroni Mhiti. 14 Baada ya kuwa amemzika babaye, Yusufu akarudi Misri, yeye, pamoja na ndugu zake, na wote waliokuwa wamemsindikiza ili kumzika babaye. 15 Nduguze Yusufu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje ikiwa Yusufu atatukasirikia na akataka kutulipa kikamilifu kwa ajili ya uovu tuliomtenda?” 16 Hivyo wakamwagiza Yusufu, kusema, “Baba yako alitoa maelekezo kabla hajafa, kusema, 17 'Mwambieni hivi Yusufu, “Tafadhari samehe makosa ya ndugu zako na dhambi yao uovu waliokutenda.” Basi wasamehe watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yusufu akalia walipomwambia. 18 Ndugu zake pia wakaenda na kuinamisha nyuso zao mbele zake. Wakasema, “Tazama, sisi ni watumishi wako.” 19 Lakini Yusufu akawajibu, “Msiogope, Je mimi ni badala ya Mungu? 20 Lakini kwenu, mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, kuhifadhi maisha ya watu wengi, kama mwonavyo leo. 21 Hivyo basi msiogope. Nitawahudumia ninyi na watoto wenu wadogo.” Kwa njia hii aliwatia moyo na kuongea na mioyo yao kwa upole. 22 Yusufu akakaa Misri, pamoja na familia ya baba yake. Akaishi miaka mia moja na kumi. 23 Yusufu akawaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu. Pia aliwaona wana wa Makiri mwana wa Manase, waliowekwa katika magoti ya Yusufu. 24 Yusufu akawambia ndugu zake, “Ninakaribia kufa; lakini kwa hakika Mungu atawajilia na kuwaongoza kutoka katika nchi hii na kuwapeleka katika nch aliyoapa kumpa Ibrahimu, kwa Isaka na kwa Yakobo.” 25 Kisha Yusufu akawaapisha watu wa Israeli kwa kiapo. Akasema, “Bila shaka Mungu atawajilia. Wakati huo mtachukuwa mifupa yangu kutoka hapa.” 26 Hivyo Yusufu akafa, mwenye miaka 110. Wakampaka dawa na akawekwa katika jeneza huko Misri.

< Mwanzo 50 >