< Mwanzo 32 >

1 Yakobo pia akaendelea na safari yake, na malaika wa Mungu wakakutana naye. 2 Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu,” hivyo akapaita mahali pale Mahanaimu. 3 Yakobo akatuma wajumbe mbele yake waende kwa Esau ndugu yake katika nchi ya Seiri, katika eneo la Edomu. 4 Aliwaagiza, kusema, “Hivi ndivyo mtakavyosema kwa bwana wangu Esau: Hivi ndivyo mtumishi wako Yakobo asemavyo: 'Nimekuwa nikikaa na Labani, naye amekawilisha kurudi kwangu hata sasa. 5 Nina ng'ombe, punda, na kondoo, wajori na wajakazi. Nimetuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili kwamba nipate kibali mbele zako.” 6 Wajumbe wakarudi kwa Yakobo na kusema, “Tulikwenda kwa Esau ndugu yako. Anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye.” 7 Ndipo Yakobo alipoogopa sana na kutaabika. Hivyo akagawanya watu aliokuwa nao katika kambi mbili, na kondoo pia, mbuzi na ngamia. 8 Akasema, “Ikiwa Esau ataishambulia kambi moja, ndipo kambi nyingine itakaposalimika.” 9 Yakobo akasema, “Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, Yahwe, uliyeniambia, 'Rudi katika nchi yako na kwa jamaa yako, nami nitakustawisha,' 10 Mimi sistahili matendo yako yote ya agano la uaminifu na ustahilifu wote uliomfanyia mtumishi wako. Kwa maana nilikuwa na fimbo tu nilipovuka mto huu wa Yordani, na sasa nimekuwa matuo mawili. 11 Tafadhari niokoe kutoka katika mikono ya ndugu yangu, mikono ya Esau, kwa maana namwogopa, kwamba atakuja na kunishambulia mimi na wamama na watoto. 12 Lakini ulisema, 'hakika nitakufanya ufanikiwe. Nitaufanya uzao wako kuwa kama mchanga wa bahari, ambao hauwezi kuhesabika kwa hesabu yake.” 13 Yakobo akakaa pale usiku huo. Akachukua baadhi ya alivyokuwa navyo kama zawadi kwa Esau, ndugu yake: 14 mbuzi majike mia mbili na mabeberu ishirini, kondoo majike mia mbili na madume ya kondoo ishirini, 15 ngamia wakamwao thelathini na wana wao, ng'ombe madume arobaini na madume kumi ya ng'ombe, punda wa kike ishirini na madume yake ishirini. 16 Akawaweka katika mikono ya watumishi wake, kila kundi peke yake. Akawambia watumishi, “Tangulieni mbele yangu na mwache nafasi kati ya makundi ya wanyama.” 17 Akamwagiza mtumishi wa kwanza, akisema, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, akasema, 'Ninyi ni wa nani? Mnakwenda wapi? Na wanyama hawa mbele yenu ni wa nani? 18 Ndipo umwambie, 'Ni wa mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi wanaopelekwa kwa bwana wangu Esau. Na tazama, yeye pia anakuja nyuma yetu.” 19 Yakobo akatoa maelekezo kwa kundi la pili pia, la tatu, na watu wote walioyafuata makundi ya wanyama. Akasema, mseme vilevile kwa Esau mtakapokutana naye. 20 Mnapaswa pia kusema, 'mtumwa wako Yakobo pia anakuja nyuma yetu.” Kwani alifikiri, “nitamtuliza Esau kwa zawadi nilizozituma mbele yangu. Kisha baadaye, nitakapomwona, bila shaka atanipokea.” 21 Hivyo zawadi zikatangulia mbele yake. Yeye mwenyewe akakaa kambini usiku huo 22 Yakobo akaamka wakati wa usiku, na akawachukua wakeze, wajakazi wake na wanaye kumi na wawili. Akawawavusha kijito cha Yaboki. 23 Kwa njia hii akawapeleka kupitia chemichemi pamoja na mali yake yote. 24 Yakobo akaachwa peke yake, na mtu akashindana naya mpaka alfajiri. 25 Mtu yule alipoona kwamba hawezi kumshinda, akalipiga paja lake. Paja la Yakobo likatenguka alipokuwa akishindana naye. 26 Yule mtu akasema, “Niache niende, kwani kunakucha.” Yakobo akasema, sitakuacha uende mpaka uwe umenibariki.” 27 Yule mtu akamwuliza, “Jina lako ni nani?” Yakobo akasema, “Yakobo.” Yule mtu akasema, 28 “Jina lako halitakuwa Yakobo tena, ila Israeli. Kwa kuwa umeshindana na Mungu na wanadamu na umeshinda.” 29 Yakobo akamwambia, “Tafadhari niambie jina lako.” Akasema, “Kwa nini kuniuliza jina langu?” Kisha akambariki pale. 30 Yakobo akapaita mahali pale Penieli kwani alisema, “Nimemwona Mungu uso kwa uso, na maisha yangu yamesalimika.” 31 Jua likatoka wakati Yakobo anaipita Penieli. Alikuwa akichechemea kwa sababu ya paja lake. 32 Ndiyo maana wana wa Israeli hawali kano ya paja iliyopo katika nyonga ya paja, kwa sababu yule mtu aliziumiza hizo kano alipotegua paja la Yakobo.

< Mwanzo 32 >