< Mwanzo 31 >

1 Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, “Yakobo amechukuwa yote yaliyokuwa ya baba yetu, na ni kutoka katika mali ya baba yetu amepata utajiri wake.” 2 Yakobo akaona mwonekano katika uso wa Labani. Akaona kwamba nia yake imebadilika. 3 Kisha Yahwe akamwambia Yakobo, “Rudi katika nchi ya baba zako na ya ndugu zako, nami nitakuwa nawe.” 4 Yakobo akatuma kuwaita Raheli na Lea uwandani katika kundi lake la kondoo 5 naye akawambia, “Naona nia ya baba yenu kwangu imebadilika, lakini Mungu wa baba yangu amekuwa nami. 6 Nanyi mnajua kwamba ni kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu. 7 Baba yenu amenidanganya na amebadilisha ujira wangu mara kumi, lakini Mungu hakumruhusu kunidhuru. 8 Ikiwa alisema, 'Wanyama wenye mabaka watakuwa ujira wako,' ndipo kondoo wote walipozaa watoto wenye mabaka. Na aliposema, wenye milia watakuwa ujira wako,' ndipo kundi lote lilipozaa watoto wenye milia. 9 Kwa njia hii Mungu amemnyang'anya mifugo baba yenu na kunipa mimi. 10 Wakati fulani wa majira ya kupandana, niliona katika ndoto mabeberu yaliyowapanda kundi. Mabeberu yalikuwa ya milia, mabaka na madoa. 11 Malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, 'Yakobo.' Nikasema, 'Mimi hapa.' 12 Akasema, 'Inua macho yako uone mabeberu wanaolipanda kundi. Wana milia, madoa na na mabaka, kwani nimeona kila jambo Labani analokutendea. 13 Mimi ni Mungu wa Betheli, mahali ulipoitia nguzo mafuta, mahali uliponitolea nadhiri. Basi sasa inuka na uondoke katika nchi hii na kurudi katika nchi uliyozaliwa. 14 Raheli na Lea wakajibu na kumwambia, “Je kuna sehemu yoyote au urithi wetu katika nyumba ya baba yetu? 15 Je hatutendei kama wageni? Kwa maana ametuuza na kwa ujumla ametapanya pesa zetu. 16 Mali zote ambazo sasa Mungu amemnyang'anya baba yetu ni zetu na watoto wetu. Sasa basi, lolote Mungu alilokuambia, fanya. 17 Kisha Yakobo akainuka na kuwapandisha wanawe na wakeze kwenye ngamia. 18 Akawaongoza mifugo wake wote mbele yake, pamoja na mali zake zote, wakiwemo wanyama aliowapata huko Padani Aramu. Kisha akaenda kuelekea kwa Isaka baba yake katika nchi ya Kanaani. 19 Labani alipokuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo wake, Raheli akaiba miungu ya nyumba ya baba yake. 20 Yakobo pia akamdanganya Labani Mwarami, kwa kutomtaarifu kwamba anaondoka. 21 Hivyo akaondoka na vyote alivyokuwa navyo na kwa haraka akavuka mto, na akaenda kuelekea nchi ya vilima ya Gileadi. 22 Siku ya tatu Labani akaambiwa kwamba Yakobo amekimbia. 23 Hivyo akawachukua ndugu zake pamoja naye na kumfuatia kwa safari ya siku saba. Akampata katika nchi ya vilima ya Gileadi. 24 Basi Mungu akaja kwa Labani Mwarami katika ndoto usiku na kumwambia, “Ujiadhari kumwambia Yakobo jambo lolote liwe jema au baya.” 25 Labani akampata Yakobo. Basi Yakobo alikuwa amepiga hema yake katika nchi ya vilima. Labani pia akapiga kambi pamoja na ndugu zake katika nchi ya kilima ya Gileadi. 26 Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini, kwamba umewachukua binti zangu kama mateka wa vita? 27 Kwa nini umekimbia kwa siri na kunihadaa kwa kutokuniambia? Ningekuruhusu uondoke kwa sherehe na kwa nyimbo, kwa matari na vinubi. 28 Haukuniacha niwabusu wajukuu wangu na binti zangu kwa kuwaaga. Basi umefanya upumbavu. 29 Iko katika uwezo wangu kukudhuru, lakini Mungu wa baba yako alisema nami usiku wa leo na kuniambia, 'Jiadhari usimwambie Yakobo neno la heri wala shari.' 30 Na sasa, umeondoka kwa sababu umeitamani sana nyumba ya baba yako. Lakini kwa nini umeiba miungu yangu? 31 Yakobo akajibu na kumwambia Labani, “Ni kwa sababu niliogopa na kudhani kuwa ungeninyang'anya binti zako kwa nguvu ndiyo maana nikaondoka kwa siri. 32 Yeyote aliyeiiba miungu yako hataendelea kuishi. Mbele ya ndugu zetu, onesha chochote kilichochako nilichonacho na uchukue.” Kwa maana Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameviiba. 33 Labani akaingia katika hema ya Yakobo, katika hema ya Lea, na katika hema za wale wajakazi wawili, lakini hakuviona. Akatoka katika hema ya Lea na kuingia katika hema ya Raheli. 34 Basi Raheli alikuwa ameichukua miungu ya nyumbani, na kuiweka katika ngozi ya ngamia, na kukaa juu yake. Labani akatafuta katika hema yote, lakini hakuiona. 35 Akamwambia baba yake, “Usikasirike, bwana wangu, kwamba siwezi kusimama mbele yako, kwani nipo katika kipindi changu.” Hivyo akatafuta lakini hakuiona miungu ya nyumbani mwake. 36 Yakobo akakasirika na kuojiana na Labani. Akamwambia, “Kosa langu ni nini? Dhambi yangu ni ipi, hata ukanifuatia kwa ukali? 37 Kwa maana umechunguza mali zangu zote. Umeona nini kati ya kitu chochote cha nyumbani mwako? Viweke hapa mbele ya ndugu zetu, ili waamue kati yetu wawili. 38 Kwa miaka ishirini nimekuwa nawe. Kondoo wako na mbuzi wako hawakutoa mimba, wala sikula dume lolote la kondoo katika wanyama wako. 39 Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea. Badala yake, nilichukua upotevu huo, kwamba wameibwa mchana au usiku. 40 Nilikuwepo wakati wote; mchana joto lilinipata, na baridi wakati wa usiku; na sikupata usingizi. 41 Miaka hii ishirini nimekuwa katika nyumba yako. Nilikufanyia kazi miaka kumi na nne kwa ajili ya binti zako wawili, na miaka sita kwa ajili ya wanyama wako. Umebadili ujira wangu mara kumi. 42 Isipokuwa Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu, yule Isaka anayemwofu, amekuwa nami, bila shaka sasa ungenipeleka mikono mitupu. Mungu ameliona teso langu na jinsi nilivyofanya kazi kwa bidii, na hivyo akakukemea usiku wa leo. 43 Labani akajibu na kumwambia Yakobo, “Mabinti hawa ni mabinti zangu, wajukuu ni wajukuu wangu, na wanyama ni wanyama wangu. Yote uyaonayo ni yangu. Lakini nitafanya nini leo kwa hawa binti zangu, au kwa watoto wao waliowazaa? 44 Hivyo sasa, na tufanye agano, wewe nami, na liwe shahidi kati yangu nawe.” 45 Hivyo Yakobo akachukua jiwe na kuliweka kama nguzo. 46 Yakobo akawambia ndugu zake, “Kusanyeni mawe.” Hivyo wakachukua mawe na kufanya rundo. Kisha wakala pale kati ya lile rundo. 47 Labani aliliita Yega Saha Dutha, lakini Yakobo akaiita Galeedi 48 Labani akasema, “Rundo hili ni shahidi kati yangu nawe leo.” Kwa hiyo jina lake likaitwa Galedi. 49 Inaitwa pia Mispa, kwa sababu Labani alisema, “Yahwe na atuangalie mimi nawe, tunapokuwa hatuonani. 50 Ikiwa utawatesa binti zangu, au ikiwa utachukua wanawake wengine mbali na binti zangu, japokuwa hakuna mwingine yupo nasi, tazama, Mungu ni shahidi kati yangu nawe.” 51 Labani akamwambia Yakobo, Tazama rundo hili, na tazama nguzo, nililoliweka kati yako nami. 52 Rundo hili ni shahidi, na nguzo ni shahidi, kwamba sitapita rundo hili kuja kwako, na kwamba wewe hautapita rundo hili kuja kwangu, kwa madhara. 53 Mungu wa Ibrahimu, na mungu wa Nahori, miungu ya baba zao, waamue kati yetu.”Yakobo akaapa kwa Hofu ya Isaka baba yake. 54 Yakobo akatoa sadaka juu ya mlima na akawaita ndugu zake kula chakula. Walikula na kukaa usiku kucha juu ya mlima. 55 Labani akaamka asubuhi na mapema, akawabusu wajuu zake na binti zake na kuwabariki. Kisha Labani akaondoka na kurudi kwake.

< Mwanzo 31 >