< Mwanzo 25 >

1 Abraham akaoa mke mwingine; jina lake aliitwa Ketura. 2 Akamzalia Zimrani, Jokshani, Medani, Midiani, Ishbaki, na Shua. 3 Jokshani akamzaa Sheba na Dedani. Wana wa Dedani walikuwa ni Waashuru, Waletushi, na Waleumi. 4 Wana wa Midiani walikuwa ni Efa, Eferi, Hanoki, Abida, na Eldaa. Hawa wote walikuwa ni wana wa Ketura. 5 Abraham akampatia Isaka vitu vyote alivyokuwa navyo. 6 Ingawaje, wakati alipokua angali akiishi, aliwapatia zawadi wana wa masuria wake na kuwapeleka katika nchi ya mashariki, mbali na Isaka, mwanae. 7 Hizi ndizo zilikuwa siku za miaka ya uhai wake Abraham alizoishi, miaka 175. 8 Abraham akapumua pumzi ya mwisho na akafa katika uzee mwema, mzee aliye shiba siku, na akakusanywa kwa watu wake. 9 Isaka na Ishmaili, wanae wakamzika katika pango la Makipela, katika shamba la Efron mwana wa Soari Mhiti, pango lililokuwa karibu na Mamre. 10 Shamba hili Abraham alilinunua kwa watoto wa Hethi. Abraham akazikwa pale pamoja na Sara mkewe. 11 Baada ya kifo cha Abraham, Mungu akambariki Isaka mwanae, na Isaka akaishi karibu na Beerlalahairoi. 12 Na sasa hawa ndio walikuwa wana wa Ishimaeli, mwana wa Abraham, ambaye Hajiri Mmisri mtumishi wake Sara, alizaa kwa Abraham. 13 Haya ndiyo yalikuwa majina ya wana wa Ishimaeli, kuanzia mzaliwa wa kwanza: Nebayothi - mzaliwa wa kwanza wa Ishimaeli, Kedari, Adbeeli, Mibsamu, 14 Mishma, Duma, Masa, 15 Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi, na Kedema. 16 Hawa ndio walikuwa wana wa Ishimaeli, na haya ndiyo majina yao, kwa vijiji vyao, na katika vituo vyao; Maseyidi kumi na wawili kufuatana na kabila zao. 17 Hii ndiyo ilikuwa miaka ya Ishimaeli, miaka 137: akapumua pumzi yake ya mwisho na akafa, na akakusanywa pamoja na watu wake. 18 Walioshi toka Havila mpaka Shuri, ambayo iko karibu na Misri, kuelekea Ashuru. Waliishi kwa uadui kati yao. 19 Haya ndiyo yalikuwa matukio kumuhusu Isaka, mwana wa Abraham: Abraham alimzaa Isaka. 20 Isaka alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomuoa Rebeka, binti wa ethueli Mshami wa Padani Aramu, ndugu wa Labani Mshami. 21 Isaka akamwomba Yahwe kwa ajili ya mke wake kwa sababu alikuwa tasa, na Yahwe akajibu maombi yake, Rebeka mkewe akabeba mimba. 22 Watoto hawa walipokuwa tumboni mwake wakasumbuka, naye akasema, “Kwa nini jambo hili linatokea kwangu mimi?” Akaenda kumuuliza Yahwe kuhusu jambo hili. 23 Yahwe akamwambia, “Mataifa mawili yako katika tumbo lako, na mataifa haya mawili yatatengana ndani yako. Taifa moja litakuwa lenye nguvu kuliko lingine, na yule mkubwa atamtumikia mdogo. 24 Ulipo wadia wakati wa kujifungua, tazama, kulikuwa na mapacha ndani ya tumbo lake. 25 Wakwanza akatoka akiwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. 26 Baada ya hapo ndugu yake akatoka. Mkono wake ukiwa umeshika kisigino cha Esau. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini wakati mke wake alipo wazaa hawa watoto. 27 Vijana hawa wakakua, Hesau akawa mwindaji hodari, mtu wa nyikani; lakini Yakobo alikuwa mtu mkimya, aliye tumia muda wake akiwa katika mahema. 28 Kisha Isaka akampenda Esau kwa sababu alikula wanyama ambao alikuwa anawinda, lakini Rebeka akampenda Yakobo. 29 Yakobo akapika mchuzi. Esau akaja kutoka nyikani, akiwa dhaifu kutokana na njaa. 30 Esau akamwambia Yakobo, “Nilishe mchuzi mwekundu. Tafadhari, nimechoka!” Na hii ndiyo sababu jina lake aliitwa Edomu. 31 Yakobo akasema, “Kwanza uniuzie haki yako ya mzaliwa wa kwanza.” 32 Esau akasema, “Tazama, nakaribia kufa. Ni nini kwangu haki ya mzaliwa wa kwanza?” 33 Yakobo akasema, “Kwanza uape kwangu mimi,” kwa hiyo Esau akaapa kiapo na kwa njia hii akawa ameuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa Yakobo. 34 Yakobo akampatia Esau mkate pamoja na mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka na akaenda zake. Kwa njia hii Esau akawa ameidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

< Mwanzo 25 >