< Mwanzo 2 >

1 Kisha mbingu na nchi zilimalizika, na viumbe hai vyote vilivyo jaza mbingu na nchi. 2 Siku ya saba Mungu alifikia mwisho wa kazi yake ambayo aliifanya, na kwa hiyo alipumzika siku ya saba kutoka kwenye kazi yake yote. 3 Mungu akaibarikia siku ya saba na akaitakasa, kwa sababu katika siku hiyo alipumzika kutoka kwenye kazi yake yote ambayo aliifanya katika uumbaji. 4 Haya yalikuwa ni matukio yahusuyo mbingu na nchi, wakati vilipoumbwa, katika siku ambayo Yahwe Mungu aliumba nchi na mbingu. 5 Hapakuwa na msitu wa shambani uliokuwa katika nchi, na hapakuwa na mmea wa shambani uliokuwa umechipuka, kwa kuwa Yahwe Mungu alikuwa hajasababisha mvua kunyesha juu ya nchi, na hapakuwa na mtu wa kulima ardhi. 6 Lakini ukungu uliinuka juu kutoka kwenye nchi na kuutia maji uso wote wa ardhi. 7 Yahwe Mungu aliumba mtu kutoka mavumbi ya ardhi, na akampulizia puani pumzi ya uhai, na mtu akawa kiumbe hai. 8 Yahwe Mungu aliotesha bustani upande wa mashariki, katika Edeni, na pale akamuweka mtu ambaye alimuumba. 9 Kutoka ardhini Yahwe Mungu alifanya kila mti uote ambao unapendeza na ni mzuri kwa chakula. Hii ni pamoja na mti wa uzima ambao ulikuwa katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. 10 Mto ukatoka nje ya Edeni kuitia maji bustani. Na kutoka pale ukagawanyika na kuwa mito minne. 11 Jina la ule wa kwanza ni Pishoni. Huu ni ule ambao unatiririka kupitia nchi yote ya Havila, ambapo kuna dhahabu. 12 Dhahabu ya inchi ile ni nzuri. pia kuna bedola na jiwe shohamu. 13 Jina la mto wa pili ni Gihoni. Huu unatiririka kupitia nchi yote ya kushi. 14 Jina la mto wa tatu ni Hidekeli, ambao unatiririka mashariki mwa Ashuru. Mto wa nne ni Frati. 15 Yahwe Mungu alimtwaa mtu na kumweka ndani ya bustani ya Edeni kuilima na kuitunza. 16 Yahwe Mungu alimuagiza mtu akisema, “kutoka kwenye kila mti bustanini waweza kula kwa uhuru. 17 Lakini kutoka kwenye mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa kuwa siku utakayo kula kutoka katika mti huo, utakufa hakika.” 18 Kisha Yahwe Mungu akasema, “siyo jambo jema kwamba mtu huyu lazima awe pekeyake. Nitamfanyia msaidizi anaye mfaa.” 19 Kutoka ardhini Yahwe Mungu akafanya kila mnyama wa kondeni na kila ndege wa angani. Kisha akawaleta kwa mtu huyu aone angewapatia majina gani. Jina ambalo mtu huyu alimwita kila kiumbe hai, hili ndilo lilikuwa jina lake. 20 Mtu huyu akawapatia majina wanyama wote, ndege wote wa angani, na kila mnyama wa mwitu. Lakini kwa mtu mwenyewe hapakuwa na msaidizi wa kumfaa yeye. 21 Yahwe Mungu akaleta usingizi mzito kwa mtu huyu, kwa hiyo mtu huyu akalala. Yahwe Mungu akatwaa moja ya mbavu za mtu huyu na akapafunika pale alipo chukua ubavu. 22 Kwa ubavu ambao Yahwe Mungu alichukua toka kwa mtu huyu, akafanya mwanamke na akamleta kwa mtu huyu. 23 Mwanaume akasema, “kwa sasa, huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu. ataitwa 'mwanamke,' kwa sababu ametwaliwa katika mwanaume. 24 Kwa hiyo mwanaume atawaacha baba yake na mama yake, ataungamanika na mke wake, na watakuwa mwili mmoja. 25 Wote wawili walikuwa uchi, mwanaume na mke wake, lakini hawakuona aibu.

< Mwanzo 2 >