< Mwanzo 14 >

1 Ikiwa katika siku za Amrafeli, mfalme wa shinari, Arioko, mfalme wa Elasari, Kedorlaoma, mfalme wa Elam na Tidali, mfalme wa Goimu, 2 walifanya vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, Birsha, mfalme wa Gomora, Shinabu, mfalme wa Adma, Shemeberi, mfalme wa Seboim, na mfalme wa Bela(pia ikiitwa Soari). 3 Hawa wafalme watano wa mwisho waliungana pamoja katika bonde la Sidim (pia likiitwa bahari ya chumvi). 4 Kwa miaka kumi na mbili walimtumikia Kedorlaoma, lakini katika mwaka wa kumi na tatu waliasi. 5 Kisha katika mwaka wa kumi na nne, Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja nae walikuja na kuwashambulia Warefai katika Ashteroth Karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, Waemi katika Shawe Kiriathaimu, 6 na Wahori katika mlima wao wa Seiri, mpaka El Parani iliyo karibu na jangwa. 7 Kisha wakarudi wakaja En Misifati (Pia ikiitwa Kadeshi), na kuishinda nchi yote ya Waamaleki, na pia Waamori ambao waliishi Hasasoni Tamari. 8 Kisha mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboim, na mfalme wa Bela (pia ikiitwa Soari) walikwenda na kuandaa vita 9 dhidi ya Kadorlaoma, mfalme wa Elam, Tidali mfalme wa Goim, Amrafeli, mfalme wa Shinari, Arioki, mfalme wa Elasari; wafme wanne dhidi ya wale watano. 10 Na sasa bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami, na wafalme wa Sodoma na Gomora walipokimbia, wakaanguka pale. Wale waliosalia wakakimbilia milimani. 11 Kwa hiyo adui akachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, na wakaenda zao, 12 walipoondoka, wakamchukua pia Lutu, mtoto wa ndugu yake na Abram ambaye aliishi Sodoma, pamoja na mali zake zote. 13 Mmoja ambaye alitoroka alikuja na kumwambia Abram mwebrania. Alikuwa anaishi katika mialoni ya Mamre, mwamori ambaye alikuwa ni ndugu wa Eshkoli na Aneri ambao walikuwa washirika wa Abram. 14 Abram aliposikia kuwa maadui wamemteka ndugu yake, akawaongoza wanaume waliofunzwa na kuzaliwa nyumbani mwake 318 na akawaongoza hadi Dani. 15 Akawagawanya watu wake dhidi yao usiku na kuwavamia, na kuwafukuza mpaka Hoba, ambayo iko kaskazini mwa Dameski. 16 Kisha akarudisha mali zote, pia akamrudisha ndugu yake Lutu na mali zake, pamoja na wanawake na watu wengine. 17 Baada ya Abram kurudi kutoka kumpiga Kadorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja nae, mfalme wa Sodoma akatoka kuonana nae katika bonde la Shawe (pia iliitwa bonde la mfalme). 18 Melkizedeki, mfalme wa Salem, akaleta mkate na divai. Alikuwa ni kuhani wa Mungu aliye juu sana. 19 Alimbariki akisema, “Abarikiwea Abram na Mungu aliye juu sana, muumba wa mbingu na nchi. 20 Abarikiwe Mungu aliye juu sana, ambaye amekupatia adui zako katika mikono yako.” Kisha Abram akampatia sehemu ya kumi ya kila kitu. 21 Mfalme wa Sodama akamwambia Abram, “Nipatie watu, na ujichukulie wewe mwenyewe mali.” 22 Abram akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua juu mkono wangu kwa Yahwe, Mungu aliye juu sana, muumbaji wa mbingu na nchi, 23 kwamba sitachukua uzi wala gidamu ya kiatu, au kitu chochote ambacho ni chako, 'ili kwamba usiseme, nimemfanya Abram kuwa tajiri.' 24 Sitachukua chochote isipokuwa kile ambacho vijana wamekula na sehemu za watu waliokwenda nami. Aneri, Eskoli, na Mamre na wachukue sehemu zao.”

< Mwanzo 14 >